1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi anataka uchaguzi huru na wa haki

16 Juni 2011

Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi amesema ataridhia ufanyike uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utakaosimamiwa na jumuiya ya kimataifa kwa masharti ya kutokuwepo kwa wizi wa kura.

https://p.dw.com/p/11bv3
In this image made from Libyan TV, Libyan leader Moammar Gadhafi holds a meeting with tribal leaders from eastern Libya, in Tripoli, Libya, Wednesday, May 11, 2011. (AP Photo / Libyan TV via APTN) TV OUT LIBYA OUTPicha: dapd

Kauli hiyo iliyotolewa na mtoto wa kiongozi huyo Seif al -Islam imechapishwa katika gazeti la leo la nchini Italia.

Katika mahojiano yake hayo Seif al Islam amesema uchaguzi huo ungeweza kufanyika ndani ya miezi mitatu. Katika makadirio yake ya juu pengine ingekuwa mwishoni mwa mwaka huu, huku akihakikisha uwazi katika ufanikishaji wake.

Amesema unaweza kusimamiwa na taasisi kama Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na hata Jumuiya ya Kujihami ya NATO ambayo imekuwa ikishambulia majeshi ya Gaddafi kwa mabomu.

Mtoto huyo wa Gaddafi alilisitiza kwamba jambo muhimu ni uchaguzi wa wazi, huku akijinasibu kwa kusema hana shaka kwamba umma wa Walibya utamuunga mkono baba yake. Na wanawaona waasi kama waislamu wenye msimamo mkali, magaidi na mamluki.

Aidha ameongeza kuwa baba yake atakuwa tayari kukaa chonjo endapo atashindwa uchaguzi lakini kamwe hatokwenda uhamishoni, akisisitiza kwamba amezaliwa Libya, na atazikwa nchini humo.

Präsident USA Barack Obama
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: dapd

Hakika mapigano yanaendelea, mpaka sasa inadaiwa waasi wanasonga mbele kuelekea ngome ya Gaddafi, huko mjini Tripoli, wakiwa katika uwanja wa mapigano upande wa magharibi mwa nchi hiyo.

Inaelezwa kwamba wanashikilia vijiji viwili ambavyo wanajeshi wa Gaddafi walikuwa wakivishambulia huku wakifanya jitihada za kusonga mbele zaidi.

Makundi mengine ya wapiganaji waasi kwa upande wa Mashariki mwa Libya na mji wa Misrata wanaendelea kukabiliana vikali na wanajeshi wa Gaddafi wenye zana bora za kivita.

Kamano mmoja wa waasi, Khalifa Hafter amesema" Kuna maendeleo yameweza kupatikana katika siku tatu zilizopita, hasa upande wa magharibi na pia Misrata kuna mabadiliko, Waasi wanaweza kuamua hatima ya Slitan na kufungua njia ya Tripoli"

Wakati hayo yakiendelea, Umoja wa Afrika umelionya baraza la usalama la umoja wa mataifa kwamba azimio la umoja huo la kuruhusu mashambulizi ya anga nchini Libya litasababisha hatari kubwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritania Hamady Ould Hamady amesema pasipo kuitaja moja kwa moja NATO kwamba mashambulizi yanayoendelea ni matakwa ya upande mmoja.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika ya Kusini, Maite Nkoana-Mashabane anaandaa hotuba itakayoituhumu NATO kwa kufanya mashambulizi yanayomlenga Gaddafi. Awali rais wake Jacob Zuma alisema kwamba jumuiya hiyo ya kujihami,operesheni zake zinavuka kikomo cha azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Libyen zerstörter Panzer an der Straße nach Adschdabija
Kifaru cha Libya kilichoharibiwa na NATOPicha: dapd

Katika hatua nyingine rais Barack Obama amesisitiza kwamba operesheni za Marekani dhidi ya Libya ni halali, akijibu ukosoaji wa bunge la nchi hiyo kuhusu lengo na uhalali wa ushiriki wa nchi hiyo.

Taarifa ya Ikulu ya Marekani inasema hakukuwepo haja ya kutaka ridhaa ya bunge kwa sababu jukumu la Marekani katika opresheni hiyo ilikuwa ni kuunga mkono tu.

Jitihada za upatanishi zinaendelea ambapo hivi punde ujumbe wa Urusi umewasili nchini Libya kwa ajili ya mazungumzo na serikali ya Muammar Gaddafi.

Mwandishi: Sudi Mnette// RTR/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu