1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi auawa mikononi mwa vikosi vya Baraza la Mpito

20 Oktoba 2011

Kiongozi aliyeondolewa madarakani nchini Libya, Muammar Gaddafi, ameripotiwa kuuwawa katika mji alikozaliwa wa Sirte, ikiwa muda mfupi baada ya vikosi vya Serikali ya Mpito kutangaza kuudhibiti mji huo.

https://p.dw.com/p/12w5T
Wapiganaji wa vikosi vya serikali ya mpito ya Libya vikishangiria kuuawa kwa Muammar Gaddafi.
Wapiganaji wa vikosi vya serikali ya mpito ya Libya vikishangiria kuuawa kwa Muammar Gaddafi.Picha: dapd

Hakika ameuwawa, licha ya kuwapo kukiwa na utata wa jinsi ya kifo cha kiongozi huyo kilivyotokea ambapo awali ilisemekana ametiwa mbaroni na muda mfupi baadaye kutangazwa amekufa.

Taarifa kutoka Baraza la Mpito linaloongoza nchi hiyo, zinasema umepelekwa kuhifadhiwa mafichoni kwa taratibu za kiusalama.

Inadaiwa kifo chake kimetokana na majeraha aliyoyapata katika mapigano yaliyotokea leo, ambayo yamehitimisha mapigano ya miezi minane ya kuupinga utawala wake wa miaka 42.

Vituo vya televisheni mbalimbali duniani vimeonesha picha inayodaiwa kuwa ya mwili wa kiongozi huyo wa zamani baada ya serikali ya mpito kuthibitisha kwamba ameuwawa mjini Sirte.

Hata hivyo picha hiyo ilipigwa kwa njia ya simu ya mkononi imekuwa vigumu kuithibitisha kwamba mtu huyo alikuwa akibubujikwa na damu alikuwa amekufa au amejeruhiwa.

Picha za maiti ya Gaddafi zaoneshwa

Gaddafí akiwa Umoja wa Mataifa katika uhai wake.
Gaddafí akiwa Umoja wa Mataifa katika uhai wake.Picha: picture-alliance/dpa

Katika tathimini yao Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, limesema imekuwa kawaida kwa wapiganaji wanaompinga Gaddafi kupiga picha matukio wakiwa katika uwanja wa mapambano.

Waziri wa Habari wa Baraza la Mpito, Mahmoud Shamam, akizungumza muda mfupi baada ya vikosi vyao kudhibiti mji wa Sirte, alisema serikali yake ingelitoa hukumu iliyo sawa kwa kila atakayetiwa kizuizini na ingelitenda haki. "Tutampeleka mbele ya mahakama. hatutawanyonga watu mitaani, tutatoa haki ambayo haijawahi kutolewa kwa watu wa Libya."

Kwa upande mwingine, Jumuiya ya Kujihami NATO imethibitisha kuushambulia msafara wa Gaddafi huku kukiwa na taarifa zilizokuwa na utata ikiwa aliuawa kwa mashambulizi hayo au aliuawa baada ya kukamatwa.

Msemaji wa NATO, Kanali Roland Lavoie, amesema makombora ya ndege za kivita za Jumuiya hiyo yameshambulia magari mawili yaliyokuwa sehemu ya kundi kubwa yaliyokuwa yakijaribu kufanya mbonu za namna ya kumtorosha kiongozi huyo.

Hata hivyo, mmoja wa maafisa wa ngazi za juu katika umoja huo aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake amesema hawawezi kuthibitisha kwamba kiongozi huyo ameuwawa au amekamatwa.

Kwa upande wake, kiongozi wa Baraza la Mpito, Mustafa Abdul Jalil, ametangaza kuthibitisha kifo hicho, ingawa mpaka sasa hajaeleza lini huku Waziri Mkuu wake, Mahmud Jibril, akitarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari hivi punde.

Katika operesheni hiyo, mtoto wa Gaddafi, Mu'tassim amekamatwa akiwa hai huku ripoti nyingine zikimtaja waziri wa zamani wa Ulinzi, Abu Bakr Younis, kuwa ameuwawa.

Mwandishi: Sudi Mnette/APE/RTR
Mhariri: Josephat Charo