1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi awahimiza wanawake vijana Uitalia kuingia Uislamu

31 Agosti 2010

Mualiko wa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi kwa mamia ya wanawake vijana kubadili dini na kuwa Waislamu,umegubika ziara yake ya siku mbili nchini Uitalia iliyokuwa na nia ya kuimarisha uhusiano kati ya Tripoli na Rome.

https://p.dw.com/p/P0TN
Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi(kushoto) na Waziri Mkuu Silvio Berlusconi wa Uitalia.Picha: AP

Katika sherehe iliyohudhuriwa na viongozi wa kampuni kuu za Kitaliana, wengi wao wakitaraji kupata kandarasi katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini yenye utajiri mkubwa wa mafuta,Waziri Mkuu wa Uitalia Silvio Berlusconi alisifu uhusiano wa kirafiki uliopo kati ya nchi hizo mbili.Kwa upande mwingine,Gaddafi alitoa mwito kwa Umoja wa Ulaya kutoa Euro bilioni 5 kwa mwaka kusaidia jitahada za kupambana na uhamiaji haramu. Lakini kiongozi huyo hapo awali aliwashtusha wengi alipowaalika wanawake vijana kwenye kituo cha utamaduni cha Libya na kuwahimiza kuingia katika Uislamu. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari wanawake watatu walibadili dini lakini habari hizo hazikuweza kuthibitishwa.

Lakini hii si mara ya kwanza kwa Gaddafi kufanya kitendo kama hicho. Kwani hata mwaka uliopita wakati wa ziara yake mjini Rome alifanya hivyo hivyo na hatua hiyo ilikosolewa na vyombo vya habari na upande wa upinzani serikalini na iliwafedhehesha wanasiasa wengi katika chama cha Berlusconi cha mrengo wa wastani wa kulia.

Gazeti la Il Messagero likauliza;"Je ingekuaje kama kiongozi wa nchi mojawapo ya Ulaya angekwenda Libya au nchi nyingine ya Kiislamu na angetoa mwito kwa kila mmoja kubadili dini na kuwa Mkristo? Bila shaka hiyo ingesababisha wimbi la malalamiko katika ulimwengu wa Kiislamu.

Berlusconi anatuhumiwa na waandishi wa habari wengi kuwa anaachilia mbali maadili na heshima kwa ajili ya uhusiano wa kibiashara na uwekezaji wa Libya nchini Uitalia. Uhusiano wa nchi hizo mbili umeimarika tangu mwaka 2008, baada ya Berlusconi kukubali kulipa fidia ya dola bilioni 5 kwa kuitawala kikoloni Libya mwanzoni mwa karne ya 20. Sasa, Uitalia ni mshirika mkuu wa Libya katika sekta ya biashara. Libya inasifiwa na viongozi wa kampuni za Kitaliana kama mwekezaji muaminifu, lakini Berlusconi alie na uhusiano wa karibu na Gaddafi, amekosolewa kuwa maslahi ya kiuchumi yanapewa kipaumbele kuliko masuala mengine kama vile haki za binadamu.

Viongozi wa upinzani hasa wanakosoa makubaliano yaliyotiwa saini kati ya nchi hizo mbili. Kuambatana na makubaliano hayo wanamaji wa Kitaliana wanaweza kuwakamata wahamiaji haramu wakiwa baharini na kuwarejesha Libya. Hatua hiyo vile vile imekosolewa vikali na shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa na makundi ya haki za binadamu. Kwa upande mwingine, wanasiasa wa chama cha Northern League, mshirika katika serikali ya muungano ya Berlusconi wameeleza wasiwasi wao kuhusu Libya inayodhibiti asilimia 6.7 ya hisa katika benki ya UniCredit, mojawapo ya benki kubwa kabisa nchini Uitalia.

Mwandishi: P.Martin/RTRE/AFPE

Mhariri: Othman,Miraji