1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Gaddafi kuilipua Tripoli"

Admin.WagnerD14 Julai 2011

Mjumbe maalumu wa serikali ya Urusi kuhusu Libya Mikhail Margelov, amesema Kiongozi wa Libya kanali Muammer Gaddafi ana mpango wa kufanya shambulio la kuuripua mji mkuu Tripoli iwapo utatekwa na waasi.

https://p.dw.com/p/11v0m
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: dapd

Katika mahojiano yake na gazeti la kila siku nchini Urusi la Izvesta ambayo yamechapishwa leo, Margelov amesema Gaddafi ana mpango wa kuulipua mji wa Tripoli endapo utachukuliwa na waasi. Mjumbe huyo amenukuliwa akisema kauli hiyo ameelezwa na Waziri Mkuu wa Libya, Baghdadi al-Mahmudi ambae alikutana nae mwezi uliyopita.

Pamoja na kuoneshwa na mshangao na hatua hiyo lakini pia alisema Gaddafi ana mizinga na miripuko mingi ya kutosha kutekeleza operesheni kama hiyo.

Margelov alikutana na waziri mkuu wa Libya mnamo tarehe 16 Juni mjniTripoli, baada ya kufanya mazungumzo mapema mwezi huo mjini Benghazi. Hata hivyo mjumbe huyo hakuweza kukutana na Gaddafi mwenyewe.

Urusi haikulipigia kura azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililofungua njia kwa majeshi ya kimataifa kuingia kijeshi nchini Libya na tangu wakati huo umekuwa ikikosoa operesheni hiyo pamoja na hatua ya Ufaransa kuwadondoshea waasi silaha.

Libyen Rebellen Ajdabiya Munition
Waasi nchini LibyaPicha: dapd

Mapambano yanaendelea kwa namna tofauti nchini Libya. leo asubuhi waasi wakiwa na malori na silaha nyingine nzito waliyashambulia majeshi ya serikali katika maeneo kadhaa ya Al-Qawalish. Katika mapambano kama hayo yaliyotokea jana wanajeshi watiifu kwa Gaddafi walitumuliwa.

Mpiganaji mmoja alisema " tumekuja hapa jana, tumekaa na tumesema hatutoondoka mpaka tuhakikishe kumekuwa shwari kabisa"

Hata hivyo waasi wamesema bado, wanajeshi wa Gaddafi wapo umbali mfupi kwa upande wa mashariki, na wamekuwa wakifyatua makombora usiku kucha ingawa kulipokucha waliacha.

Kuudhibiti mji wa Al-Qawalash ni hatua muhimu kimkakati, kwa kuwa inatoa fursa kwa waasi kufika eneo hilo kutoka katika ngome yao huko milimani na kufika mpaka mji wa Garyan.

Hatua hiyo itawafanya waweze kudhibiti barabara kuu kuelekea upande wa kaskazini, ukiwa ni uelekeo pekee mkubwa kwenda Tripoli.

Wakati huohuo utawala wa Gaddafi umeishutumu Jumuiya ya kujihami (NATO) kwa madai ya kufanya mauwaji ya raia 1,100 wa nchi hiyo. Utawala huo hivi sasa unataka kumfikisha katibu mkuu wa NATO, Anders Forgh Rasmussen katika mahakama ya nchi hiyo, kutokana na tuhuma za uhalifu wa kivita, uliyotokana na hujuma za mashambulizi ya anga.

Lakini Mwendesha mashitaka mkuu wa Libya, Mohamed Zekri Mahjubi aliwaambia waandishi wa habari wa kigeni kwamba nato imefanya mashambulizi mjini Tripoli na miji mingine ambapo watu kiasi ya 4,537 wamejeruhiwa.

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP/RTR

Mhariri:Abdul-Rahman