1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gadhafi aishika EU ndipo

Admin.WagnerD30 Novemba 2010

Kiongozi wa Libya, Muammar Gadhafi, anasema kwamba inachotafuta Afrika ni makubaliano yenye maslahi ya kiuchumi kati yake na Umoja wa Ulaya, kwamba huo ndio msingi wa mahusiano baina ya bara hilo na mataifa mengine.

https://p.dw.com/p/QLpn
Kiongozi wa Libya, Muammar Gadhafi (kulia) akipeana mikono na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, wakati wa mkutano wa tatu kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya, mjini Tripoli, Libya. (Picha ya AP/Geert Vanden Wijngaert)
Kiongozi wa Libya, Muammar Gadhafi (kulia) akipeana mikono na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, wakati wa mkutano wa tatu kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya, mjini Tripoli, Libya. (Picha ya AP/Geert Vanden Wijngaert)Picha: AP

Akifungua mkutano huo wa kwanza katika muda wa miaka mitatu kati ya Afrika ´na Ulaya, Kanali Gadhafi alivigusa vidonda ambavyo tayari vimekwishaanza kupona kati ya mataifa yenye historia ya mtawala na mtawaliwa katika zama za ukoloni mkongwe. Nchi nyingi za Kiafrika zilikuwa chini ya ukoloni wa mataifa ya Ulaya kwa takribani karne nzima baina ya karne ya 19 na ya 20.

Sasa ni karibuni nusu karne tangu Afrika kujipatia uhuru wake, na Gadhafi anasema kwamba jukumu kubwa la hivi sasa, ni juhudi za kupatikana ushirikiano mpya ambapo kila upande utakuwa na haki sawa. Katika hotuba yake ya dakika 45, kiongozi huyo wa miongoni mwa nchi zenye nguvu za kiuchumi katika bara la Afrika, amesema kuwa Afrika inataka uhusiano wa nipe-nikupe ulio katika msingi wa mahusiano ya usawa, na sio unyonyaji.

Kiongozi wa Libya, Muammar Gadhafi (katikati), Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman van Rompuy (kushoto) na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Gabon, Ali Bongo, wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Afrika na Ulaya mjini Tripoli, Libya, Jumatatu ya 29 Novemba, 2010. EPA/MOHAMED MESSARA
Kiongozi wa Libya, Muammar Gadhafi (katikati), Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman van Rompuy (kushoto) na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Gabon, Ali Bongo, wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Afrika na Ulaya mjini Tripoli, Libya, Jumatatu ya 29 Novemba, 2010. EPA/MOHAMED MESSARAPicha: picture-alliance/dpa

Lakini, katika hali ya kuonesha kuwa viongozi wa mabara haya wanazungumza lugha mbili tafauti, rais wa Umoja wa Ulaya, Herman van Rompuy, amejibu kwa kusema kuwa uzoefu wa bara la Ulaya katika mwelekeo wa ukuaji wa uchumi unakwenda sambaba na vigezo vya utawala bora.

Kwa miaka kadhaa, Ulaya imekuwa ikizilaumu tawala za nchi nyingi za Kiafrika kuwa si za kidemkorasia na zisizohishimu haki za binaadamu, huku viongozi wa Kiafrika nao wakizilaumu serikali za Ulaya kuwa, licha ya kuyawacha makoloni yao ya zamani kuwa na uhuru wake wa bendera, bado zimeendelea na siasa za ukoloni mamboleo

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema kwamba bado bara la Afrika lina umuhimu mkubwa kwa bara laUlaya, na hivyo mahusiano mema lazima yadumishwe baina yao.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, amesema kuwa hadi sasa, Umoja huo ndio mfadhili mkubwa wa misaada ya kibiashara kwa Afrika, ukiwa umeshatoa kiasi cha Euro bilioni 10 katika mwaka 2008 pekee.

Wakati huo huo, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyopatika kwa vyombo vya habari, leo hii Umoja wa Ulaya na mataifa ya bara la Afrika yanatarajiwa kuitaka Sudan kukubali matokeo ya kura ya maoni itakayofanyika mwakani kuamua iwapo upande wa kusini ujitenge.

Wanadiplomasia na wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kura hiyo ya Januari 9 katika eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta, inatarajiwa kuamua eneo hilo kuwa huru, lakini pia inaweza kuwa ni chanzo cha kuzuka tena kwa mzozo baina ya Kusini na Kaskazini.

Kura ya maoni ya Sudan ya Kusini ni sehemu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005, ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Khartoum na Juba.

Mwandishi: Schaeffer,Utte/ZR/Sekione Kitojo

Mhariri: Miraji Othman