1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaSri Lanka

Gari la mashindano lapinduka na kuuwa watu 7 Sri Lanka

Bruce Amani
21 Aprili 2024

Watu wasiopungua 7 wamekufa leo na wengine 21 wamejeruhiwa baada ya gari la mashindano kuparamia kundi la watazamaji waliofurika kwenye uwanja wa michezo mjini Colombo nchini Sri Lanka.

https://p.dw.com/p/4f1sr
Moja ya mashindano ya magari
Magari ya mashindano huwa na mwendokasi mkubwa. Picha: James Moy/PA/picture alliance

Duru zinasema wengi walikusanyika kutizama mbio za magari zilizoandaliwa na jeshi la nchi hiyo. Dereva wa gari mojawapo la mashindano alipoteza udhibiti na chombo hicho kuwavamia watizamaji na kisha kupinduka.

Afisa mmoja amesema jumla ya watu 27 wamepelekwa hospitali na miongoni mwa watu 7 waliokufa yumo binti wa miaka minane. Kabla ya mkasa huo Mkuu wa Majeshi wa Sri Lanka Vikum Liyanage alitoa tangazo la kuruhusu mashabiki wa mbio za magari kuingia uwanjani bila malipo.

Mashindano hayo yalikuwa ya kwanza kuandaliwa katika kipindi cha miaka mitano kutokana na mzozo wa kiuchumi na janga la virusi vya corona.