1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GARISSA:Kiongozi wa mahakama za Kiislamu za Somalia akamatwa Kenya

17 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCa0

Polisi nchini Kenya wamemkamata mmoja wa viongozi wa mahakama za Kiislamu za Somalia.Kiongozi huyo alikamatwa katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyo karibu na mpaka wa Kenya na Somalia kulingana na duru za polisi.Viongozi wa ngazi za juu wa mahakama hizo Sheik Hassan Dahir Aweys na Sheik Sharif Sheik Ahmed wanashikilia kuwa wataendelea na mapigano mpaka pale majeshi ya Ethiopia yatakapoondoka nchini Somalia.Katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita wapiganaji ambao hawajatambuliwa wameshambulia mara kadhaa majeshi ya Ethiopia yaliyo mjini Mogadishu.Sheik Aweys ndiye mwanzilishi wa mahakama hizo za kiislamu zinazongangania Somalia kuwa taifa linalofata sheria za kiislamu za Sharia.

Somalia imekumbwa na mapigano katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita pale mahakama hizo za kiislamu zilipoanza kusababisha vurugu.Rais wa Somalia Abdillahi Yusuf aliagiza majeshi ya nchi jirani ya Ethiopia kuunga mkono majeshi yake ili kupambana na mahakama hizo.

Wakati huohuo Shirika la IGAD linatoa wito kwa mataifa nane wasio wanachama kuchangia majeshi ya kulinda nchini Somalia.Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa umeidhinisha kikosi cha majeshi alfu 8 kupelekwa nchini humo japo Somalia yenyewe inapinga pendekezo hilo.

Shirika la IGAD limetoa wito huo kwa mataifa ya Angola,Msumbiji,Nigeria,Rwanda,Afrika Kusini,Tanzania,Tunisia na Zambia kuchangia katika kikosi cha kulinda amani kinachopangiwa kupelekwa Somalia baada ya majeshi ya Somalia na Ethiopia kufurusha wapiganaji wa mahakam za kiislamu.Mpango mzima wa kupeleka majeshi ya kulinda amani nchini Somalia uliidhinishwa na Shirika la IGAD miaka miwili iliyopita.Mwenyekiti wa shirika hilo Rais Mwai Kibaki wa KENYA amewaagiza wajumbe sita maalum kutoka mataifa wanachama kutathmini uwezekano wa kuongeza idadi ya majeshi ya kulinda amani.