1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gates ziarani Iraq

Maja Dreyer20 Aprili 2007

Kwenye ziara yake nchini Iraq, waziri ya ulinzi wa Marekani, Robert Gates, alirudia dai la serikali yake kwa serikali ya Iraq kuitaka iongeze juhudi zake za kutafuta maridhiano ya kitaifa. Gates pia alitetea mkakati mpya wa Marekani ambao ulikosolewa na seneta maarufu Reid wa chama cha Demokratik ambaye alisema Marekani imeshindwa katika vita hivi vya Iraq.

https://p.dw.com/p/CB4Y
Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq
Wanajeshi wa Marekani nchini IraqPicha: AP

Ni ziara yake ya tatu nchini Iraq, ujumbe wake mkuu lakini ubaki kuwa ni mmoja. Waziri wa ulinzi Robert Gates wa Marekani anaitaka Iraq izidishe kazi katika mradi wa kuleta maridhiano kati ya Wasuni na Washia.

Baada ya kukutana na waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, Gates alisema alimuomba al-Maliki ambaye ni wa jamii ya Kishia ambao ni wengi nchini Iraq, kushirikiana na Wasuni na kugawa utawala ili kumaliza mivutano ya kidini. Tayari kabla ya kukutana na viongozi wa Iraq, Bw. Gates aliwaonya Wairaqi kuwa subira ya Marekani ina mwisho wake. Mbele ya waandishi wa habari wanaomsindikiza, waziri Gates alisema anataka sheria muhimu zipitishwe haraka ambazo zinahusu ugawaji wa mapato ya kuuza mafuta pamoja na kusitisha amri za kupiga marufuku wanachama wa zamani wa chama cha Saddam Hussein kufanya kazi ya serikali tena. Waziri Gates: “Kusema ukweli, ningependa kuona mambo yanaendelea haraka zaidi. Si kwamba sheria zinaweza kubadilisha hali moja kwa moja lakini uwezo tu wa kuzipitisha unaonyesha kuna nia ya kushirikiana, yaani pande zote za serikali ya Iraq zinaanza kutatua alau baadhi ya matatizo yaliyopo.”

Gates alisema bunge la Iraq linapaswa kupitisha sheria hizo fulani kabla ya kuanza kipindi cha mapumziko mwezi wa Juni na aliongeza kusema kuwa mafanikio katika kuleta maridhiano yatakuwa muhimu katika ukaguzi wa Marekani juu ya mkakati wake wa kijeshi baadaye mwaka huu.

Matamshi ya Robert Gates ni matamshi makali zaidi kutoka upande wa Marekani kuishurutisha serikali ya Iraq. Gates alisema kuwa mkakati wa Marekani kupeleka wanajeshi zaidi ili kupiga vita wanamgambo haulengi tu katika kuleta usalama bali pia kuipa serikali ya Iraq nafasi ya kuendelea kisiasa.

Kufuatia mkutano na wakuu wa majeshi na waziri wa ulinzi wa Iraq, Gates alitetea mkakati huo dhidi ya ukosoaji uliotajwa na seneta maarufu wa chama cha Demokratik cha Marekani, Harry Reid, ambaye alisema Marekani imeshindwa nchini Iraq. Si jambo la kushangaza kuwa matokeo si mazuri, alieleza Gates akitaja mashambulio makubwa yaliyotokea wiki hii ambapo watu wasiopungua 200 waliuawa. Tunataraji tutakabiliana na hali ngumu, alisema Gates na kukanusha matamshi ya seneta Reid kwamba Marekani imeshindwa.

Mjini Washington, serikali ya Marekani ya rais Bush imeingia katika hali ya mgongano kati yake na Chama cha Demokratic chenye wingi katika bunge unaohusu fedha za kugharamia hatua hiyo ya dharura. Wademokratik wanataka kuwekwa tarehe ya kuondosha majeshi kutoka Iraq, lakini rais Bush alisema atalipinga hilo kwa kutumia kura ya turufu.

Leo hii, maseneta wa jimbo la Vermont, Marekani, walipitisha azimio kuhusu kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais Bush na makamu wake waziri Dick Cheney. Azimio hilo linasema sera za Bush na Cheney ndani ya Marekani na nje, pia kuhusiana na Iraq, zinaleta wasiwasi juu ya iwapo hatua zilizochukuliwa zinaenda sambamba na katiba na ni za kutumia vibaya imani ya umma.