1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gauck : Wajibu wa uadilifu kuwaokowa wahamiaji

22 Juni 2015

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani ametowa wito wa kuwepo kwa huruma zaidi katika suala la kuwashughulikia wahamiaji na kwamba suala la kuwapatia hifadhi wahamiaji hao halina mjadala.

https://p.dw.com/p/1FkBZ
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani na Asma Abubaker Ali aliyekimbia kutoka Afrika Kaskazini wakiwa mjini Berlin. (20.06.2015)
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani na Asma Abubaker Ali aliyekimbia kutoka Afrika Kaskazini wakiwa mjini Berlin. (20.06.2015)Picha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Akizungumza Jumamosi (20.06.2015) katika hafla mjini Berlin mji mkuu wa Ujerumani kuwakumbuka wahanga waliopotezewa makaazi yao, Gauck amesema anatumai kwamba kumbukumbu ya Wajerumani waliotimuliwa ambao walilazimika kukimbia maeneo ya mashariki yaliokuwa chini ya udhibiti wa Ujerumani wakati na baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia itazidi kuimarisha uwelewa wa suala la wahamiaji hivi leo.

Ameelezea jinsi Wajerumani milioni 12 hadi milioni 14 walivyopoteza makaazi yao kufikia mwishoni mwa vita hivyo na kupelekea ongezeko la asilimia ishirini ya idadi ya watu katika ziliokuwa Ujerumani ya magharibi na mashariki hapo zamani.

Gauck amesema Ujerumani iliweza kuwajumuisha kwenye jamii mamilioni ya wakimbizi miaka sabini iliopita wakati ilipokuwa "maskini na ilipokuwa imeharibiwa vibaya" kwa hiyo inapaswa kuweza kufanya mengi zaidi katika suala la mzozo wa wakimbizi hivi sasa na hata kunufaika nalo.

Dhima ya wakimbizi

Rais huyo wa Ujerumani ameuliza kwa nini Ujerumani yenye mafanikio ya kiuchumi na ilio imara kisiasa ishindwe kutambuwa fursa za usoni zinazotokana na changamoto za hivi sasa.?

Ametaka "tukumbuke dhima kubwa waliotimiza wakimbizi na wahamiaji katika kuijenga Ujerumani kwa mafanikio."

Rais Gauck pia ametowa wito kwa nchi zinazounda Umoja wa Ulaya kuchukuwa hatua zaidi kusaidia kukabiliana na wimbi la wakimbizi linalozidi kukuwa kukimbilia Ulaya.

Wajibu wa uadlifu

Kutokana na idadi kubwa ya wahamiaji ambao wamepoteza maisha yao wakati wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterenia kwa maboti kutoka Afrika kuja Ulaya, Gauck amesema ni "wajibu wa uadlifu "kuwaokowa watu wasizame.

Rais Joachim Gauck akizungumza mjini Berlin. (20.06.2015)
Rais Joachim Gauck akizungumza mjini Berlin. (20.06.2015)Picha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Amesema watapoteza heshima ya kujiheshimu iwapo watawaacha watu waelee baharini na kujiokowa wenyewe karibu na bara lao na kuongeza kwamba mataifa yote ya Ulaya yana wajibu wa kuwapatia watu hao hifadhi.

Akifafanuwa zaidi Gauck amesema wajibu huo hauna mjadala na unadumu hadi pale wahamiaji aidha wanakuwa wanaweza kurudi nyumbani bila ya hatari yoyote ile au wanakuwa wamepata mahala wanapoweza kuishi kwa usalama iwe nchini Ujerumani au mahala kwengine.

Hakuna ufumbuzi mwepesi

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere pia alihudhuria hafla hiyo na kutowa onyo kwamba "hakuna ufumbuzi rahisi " katika mzozo huo wa wahamiaji uliopo hivi sasa.

Mwaka jana serikali ya Ujerumani ilitangaza Juni 20 kuwa ni siku ya kumbukumbu kwa wakimbizi na watu waliopotezewa makaazi yao kwa kwenda sambamba na Siku ya Wakimbizi Duniani inayoadhimishwa na Umoja wa Mataifa.

Kwa Ujerumani siku hii kwa kiasi fulani ni kumbukumbu ya kuwakumbuka mamilioni ya Wajerumani ambao walilazimika kukimbia makaazi yao katika nchi kadhaa za Ulaya ya mashariki kutokana na Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kutafuta hifadhi nchini Ujerumani na Austria na kupelekea ongezeko kubwa la idadi ya watu katika nchi hizo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP, dpa, KNA,

Mhariri : Caro Robi