1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza hali ni ngumu

Mohamed Abdul-Rahman23 Januari 2008

Maelfu waingia Misri kununua bidhaa muhimu baada ya wanaharkati kuuripua mpaka.

https://p.dw.com/p/CwP3
Wakaazi wa Gaza wakivuka mpaka kuingia Misri.Picha: AP

Maelfu ya wapalestina wameuhama ukanda wa Gaza leo na kuingia Misri, kupitia matundu kadhaa yaliotokana na ukuta ulioripuliwa na nyaya zilizokatwa , katika mpaka wa Misri na eneo hilo la Wapalestina. Mashahidi walisema ukuta huo uliripuliwa na wanaharakati waliokua na silaha na nyuso zilizovunikwa kwa kitambaa.

Matukio haya yanafuatia mapigano makali kati yxa askari wa usalama wa Misri na maelfu ya wafuasi wa chama cha Hamas,katika kituo cha kuvukia mpakani cha Rafah. Hata hivyo leo Walinzi hao wa mpakani wa Misri hawakuingilia kati na badala yake wakawaruhusu wapalestina kuingia wakielekea al Arish katika eneo la pwani la kilomita 50 kusini mwa Gaza, kununua chakula, mafuta na mahitaji mengine muhimu.

Baadhi yao walionekana wakirudi Gaza wakiwa na vikabu na bidhaa nyengine migongoni. Mmoja wao alikua na bastola saba ambazo zilitaifishwa na wanaharakati wa Hamas.

Wanaharakati hao waliokua na silaha, kutoka tawi la kijeshi la chama cha Hamas, linalojulikana kama kikosi cha al-Qassam pamoja na kamati za umma za upinzani dhidi ya Israel, walionekana wakiondoa mabaki ya vifusi vya ukuta huo katika mpaka wa Gaza na Misri kufungua njia ya kupita wapalestina.

Maelfu ya wakaazi wa Gaza wamo katika hali ngumu ya kiuchumi iliosababishwa na hatua ya Israel ya kulifunga eneo hilo, kufuatia hujuma za makombora ya wapalestiana ndani ya Israel.

Jana asubuhi Israel ilivifungua vituo viwili katika mpaka wake na Gaza kuruhusu misaada ya kiutu na mafuta ya diesel baada ya karibu siku nne za kufungwa kabisa kwa eneo hilo, katika kile kilichoonekana kuwa ni “wa ndani ndani na wa nje kusalia nje.“

Mafuta hayo lakini yanatosha tu kwa matumuzi ya wiki moja kwa ajili ya umeme na shughuli za hospitali. Lakini Israel imekula kiapo kuendelea na hatua yake ya kulibana eneo hilo hadi wanaharakati wa kipalestina wamesitisha mashambulizi ya maroketi dhidi ya Israel.

Wakati huo huo mashirika ya misaada ya kimataifa yameonya juu ya hatari ya kuzuka janga la binaadamu ikiwa Israel itaendelea na hatua yake ya kulifunga eneo la Gaza.

Jana baraza la usalama la umoja wa mataifa lilikutana kwa dharura kuijadili hali ya mambo, huku Libya inayoshikilia wenyekiti wa baraza hilo mwezi huu, ikiwasilisha muswada utakaoitaka Israel isitishe hatua yake hiyo na kuhakikisha misaada ya binaadamu inawafikia wapalestina.

Hata hivyo balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Zalmay Kalilzad aliwaambia waandishi habari kwamba muswaada huo jinsi ulivyo hivi sasa haukubaliki, kwa sababu hautaji juu ya hujuma za maroketi zinazofanywa na wanaharakati wa kipalestina dhidi ya Israel.