1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA : Hamas yamshutumu Abbas kutaka kufanya mapinduzi

17 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCif

Hamas imemshutumu Rais Mahmoud Abbas wa Palestina kwa kutaka kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya Palestina inayongozwa na kundi hilo baada ya rais huyo kutangaza mpango wa kuitisha uchaguzi na mapema.

Hamas imesema rais huyo hana mamlaka ya kuitisha uchaguzi na mapema na kwamba alikuwa anafanya mapinduzi. Viongozi wa kundi hilo wamesema kamwe hawatokubali kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi huo na mapema lakini hawakusema watauzuwiya kwa njia gani.

Abbas ameutetea uamuzi wake wa kuitisha uchaguzi huo kwa kusema kwamba ana mamlaka ya kuitimuwa serikali.Pia amesema hatoruhusu hali mbaya ya Palestina kugeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Rais huyo wa Palestina amesema uchaguzi huo unapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo lakini ameongeza kusema kwamba juhudi za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa zinapaswa kuendelea.

Kulikuwa na mapigano ya hapa na pale wakati maelfu kwa maelfu ya wafuasi wa Hamas na wale wa kundi la Fatah la Rais Abbas walipomiminika katika mitaa ya Gaza na Ukingo wa Magharibi kufuatia hotuba yake hiyo.

Serikali ya Marekani imeikaribisha hotuba hiyo ya Abbas na Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair ambaye anatazamiwa kukutana na Abbas hivi karibuni akiwa kwenye ziara yake ya Mashariki ya Kati ameitaka jumuiya ya kimataifa kumuunga mkono Abbas kwa kuitisha uchaguzi wa mapema.

Takriban watu sita wamejeruhiwa katika mapambano kati ya wafuasi wa makundi hayo mawili huko Gaza.