1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza na Ukraine Magazetini

28 Julai 2014

Vita vya Gaza,biashara ya silaha,mzozo wa Ukraine na mkataba wa Bonn,miaka 15 tangu serikali kuu ya Ujerumani ilipohamia Berlin ni miongoni mwa mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

https://p.dw.com/p/1CjsE
Shambulio la jeshi la wanaanga la Israel dhidi ya GazaPicha: Reuters

Tuanzie moja kwa moja mashariki ya kati ambako juhudi za kimataifa kuhakikisha silaha zinawekwa chini mpaka sasa hazikuleta tija. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaandika:"Vurugu za kidiplomasia zilizoachwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani ni kubwa. Wiki nzima John Kerry alijitahidi kupatanisha katika vita vya Gaza; mwishoni mwa wiki amerejea Washington mikono mitupu. Jana jumapili hakuna yeyote huko Gaza aliyekuwa akijua kama mpango wa kuweka chini silaha utaheshimiwa au vikosi vipi vitakuwa vya mwanzo kufyetua mizinga. Licha ya kuungwa mkono wa Umoja wa mataifa, Umoja wa Ulaya na serikali kadhaa,mpango wa Kerry, uliokuwa umewekewa matumaini makubwa-ya kuwekwa chini silaha kwa muda wa wiki moja na wakati huo huo kupatikana fursa ya kuanzishwa mazungumzo,umesalia karatasini tu. Jumuia ya kimataifa haijui ifanye nini-wiki nne tangu vita kuanza,watu zaidi ya elfu moja wameshapoteza maisha yao.

Damu inamwagika pia Ukraine

Vita vinapamba moto pia katika eneo la Mashariki la Ukraine kati ya vikosi vya serikali ya Ukraine na wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi. Matumaini ya kuufumbua kwa njia za amani mzozo huo nayo pia ni finyu. Gazeti la "Süddeutsche" linaandika:"Waziri mkuu Arsenyi Yazenyuk alitoa maneno makali alipotangaza kujiuzulu alkhamisi iliyopita-serikali yake ya muungano inazozana. Lakini yote haya yanafungua njia ya kuchaguliwa bunge jipya. Hatua hii ilikuwa ichukuliwe zamani. Baada ya kuchaguliwa Petro Poroschenko kuwa rais wa Ukraine,uchaguzi wa bunge ingekua hatua ya pili muhimu katika utaratibu wa kugawa upya madaraka katika nchi hiyo inayozongwa na misuko suko.

Ukraine Lugansk Zerstörung mit Artillerie zivile Opfer Zivilisten Kinder
Wahanga wa mashambulio ya LuganskPicha: picture-alliance/dpa

Eti vikwaazo ndio dawa?

Vita Mashariki ya Ukraine ndio chanzo cha miito inayotaka Urusi iwekewe vikwazo zaidi vya kiuchumi kutokana na dhana nchi hiyo inawaunga mkono waasi wanaopigania kujitenga eneo hilo.Gazeti la "Main Post" linaandika:"Udanganyifu,hadaa na uwongo-yote hayo yanabidi yasite hivi sasa. Vikwazo vya kiuchumi vinabidi vimuathiri vibaya sana Putin. Na cha kutangulizwa mbele zaidi ni silaha. Na hasa teknolojia ya nchi za magharibi ambayo Urusi inaihitaji ili kuchimba mali ghafi iliyoko chini ya ardhi yake. Mapato yanayowatajirisha wenye kumiliki makampuni ya mafuta na kuifanya serikali iyatumie kuwatuliza wananchi. Na pia soko la fedha lizingatiwe. Wajasiria mali wa Urusi wanahitaji mikopo. Dala bilioni 155 wameshakopa hadi sasa toka benki za Ulaya. Vizuwizi katika kuwapatia mikopo vinaweza kuwasababishia madhara makubwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir.

Mhariri: Josephat Charo