1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA: Rais Abbas akutana na waziri mkuu Haniyeh

23 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBz4

Rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, wa chama cha Fatah amekutana na waziri mkuu, Ismail Haniyeh, wa chama cha Hamas mjini Gaza hii leo katika juhudi za kuyafufua makubaliano ya kusitisha mapigano baina ya Palestina na Israel.

Makubaliano hayo yalivunjika wakati wanamgambo wa kundi la Hamas walipoanza kuvurumisha maroketi kuelekea Israel.

Rais Abbas na waziri mkuu Haniyeh wamekutana kwa mara ya kwanza tangu mapigano baina ya Hamas na Fatah yalipozuka wiki mbili zilizopita. Wapalestina zaidi ya 50 waliuwawa kwenye mapigano hayo.

Makundi hayo hasimu yalifikia makubaliano ya kusitisha mapigano mwishoni mwa juma lililopita, lakini hali ya wasiwasi inaendelea kuzidi kwa kuwa mzozo juu ya vikosi vya usalama haujatanzuliwa.

Ahmed Youssef, ambaye ni mpambe wa waziri mkuu Haniyeh, amesema makubalino baina ya Palestina na Israel sharti yajumulishe eneo la Ukanda wa Gaza na ukingo wa magharibi wa mto Jordan.

Mkataba wa mwezi Novemba mwaka jana ulihusu mpaka kati ya Israel na Gaza na Israel imekataa masharti ya Palestina iache kuwavamia washukiwa na kuwakamata katika eneo la ukingo wa magharibi wa mto Jordan.