1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA:Makundi hasimu yaahidi kusitisha ghasia

15 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC1x

Makundi hasimu ya Palestina yanaahidi kushirikiana ili kumaliza ghasia mjini Gaza kufuatia ongezeko la vita katika kipindi cha miezi michache iliyopita. Mazungumzo kati ya kundi la Hamas na Fatah yalifanyika baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani kujiuzulu.Kiongozi huyo alikuwa na jukumu la kusimamia majeshi ya usalama ili kujaribu kupoza ghasia zinazohofiwa kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Saa chache baada ya makundi hayo kukutana,mpiganaji mmoja wa Hamas alipigwa risasi hadi kufa huku ghasia zikiendelea katika eneo hilo kwa mujibu wa wahudumu wa hospitali.Wapalestina wane wakiwemo wapiganaji wawili walikufa katika mapigano yaliyozuka awali.

Watu 10 wameuawa mjini Gaza tangu mapigano mapya kuanza tangu Ijumaa na kusababisha hofu kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe huenda vikachipuka.Makundi ya Palestina yalifikia makubaliano ya kusitisha vita miezi kadhaa iliyopita.

Waziri wa mambo ya Ndani Hani al Qawasmi alijiuzulu kwasababu ya mivutano kati yake na Fatah kuhusiana na usimamizi wa majeshi ya usalama kulingana na maafisa wa serikali.Majukumu ya kiongozi huyo yanatekelezwa na Kiongozi wa Hamas aliye pia Waziri Mkuu.Viongozi wa pande zote mbili wanakubaliana kuondoa wapiganaji wao mjini Gaza.

Hatua ya Waziri wa mambo ya ndani kujiuzulu inapelekea tashwishi hususan kuendelea kwa ugavi wa madaraka kati ya Hamas na Fatah.Pande zote mbili ziliafikiana kuondoa wapiganaji wao mjini Gaza kabla ya Wapalestina kuadhimisha Naqba….ambayo ni kumbukumbu ya matatizo yaliyowakumba baada ya kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 48.Kwa upande mwingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Tzipi Livni anasisitiza kuwa Kundi la Hamas haliko tayari kufanya mazungumzo kuhusu suala la kuunda taifa la Palestina.