1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gbagbo afunguliwa rasmi mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu

Mohammed Khelef/AFP/AP30 Novemba 2011

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imemfungulia rasmi mashitaka aliyekuwa rais wa Cote d'Ivoire, Laurent Gbagbo, siku moja tu baada ya kufikishwa kwenye mahabusu za mahakama hiyo mjini The Hague Uholanzi.

https://p.dw.com/p/13JqA
Aliyekuwa rais wa Cote d'Ivoire, Laurent Gbagbo
Aliyekuwa rais wa Cote d'Ivoire, Laurent GbagboPicha: picture alliance/abaca

Gbagbo amefunguliwa mashitaka manne, yakiwemo mauaji, ubakaji na uhalifu dhidi ya binaadamu, anayoshukiwa kuyafanya wakati wapiganaji wake wakipambana kumbakiza madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka jana.

Katika taarifa yake ya leo, mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Luis Moreno-Ocampo amesema kwamba Gbagbo anashitakiwa kwa jukumu lake binafsi katika mashambulizi dhidi ya raia yaliyofanywa na vikosi vyake kwa niaba yake.

Kwa mujibu wa hati za mahakama, Gbagbo anashitakiwa kama mtekelezaji asiye wa moja kwa moja, katika kampeni iliyopangwa vyema ya vurugu dhidi ya raia waliochukuliwa kuwa ni wafuasi wa rais wa sasa Alassane Ouatarra. Waendesha mashtaka wanasema kiasi ya watu 3,000 waliuawa katika vurugu zilizofanywa na pande zote mbili baada ya uchaguzi.

Ocampo amesisitiza kwamba pande zote mbili katika mgogoro wa Cote d'Ivoire zilifanya uhalifu dhidi ya ubinaadamu, na kwamba bado uchunguzi unaendelea. Kauli hii inatajwa kuzungumzia wasiwasi uliopo kwamba kukamatwa kwa Gbagbo kutachochoea machafuko nchini humo, kwa kuwa kunatoa sura ya ushindi kwa upande wa Rais Alassane Ouattara dhidi ya ule wa Gbagbo.

Mwendesha Mashataka wa ICC, Luis Moreno-Ocampo
Mwendesha Mashataka wa ICC, Luis Moreno-OcampoPicha: Picture-Allianc/dpa

Msemaji wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, Reed Brondy, amesema kwamba mashitaka dhidi ya Gbagbo ni nusu tu ya hadithi yote, kwani wale waliotenda uhalifu kwa upande wa Gbagbo bado hawakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Brondy amesema na hapa namnukuu: "Hili linajenga hoja ya ushindi kwa mwenye nguvu. Na ikiwa tunataka mzunguko wa fujo umalizike nchini Cote d'Ivoire, lazima kuwa na haki kwa pande zote mbili." Mwisho wa kumnukuu.

Hata hivyo, Brody amesema kwamba kukamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa Gbagbo ni somo kwa viongozi wengine wa kisiasa na kijeshi walioko madarakani, kwamba hatimaye hawataweza kuepuka mkono wa sheria.

Mapema asubuhi ya leo, msafara wa magari uliomchukuwa Gbagbo ulielekea kwenye mahabusu ya ICC, kaskazini mwa Uholanzi, baada ya kumchukuwa kutoka ndege ya Shirika la Ndege la Cote d'Ivoire, iliyokuwa imembeba.

Gbagbo, mwenye miaka 66, ni rais wa kwanza wa zamani na mtuhumiwa wa sita kuwekwa mahabusu na mahakama hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2002, ingawa waendesha mashitaka walishawahi kufungua mashitaka dhidi ya Rais Omar al-Bashir wa Sudan kwa mauaji ya maangamizi na marehemu Muammar Gaddafi, kwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Hadi sasa, ICC imeanzisha uchuguzi wa washukiwa saba, wote kutoka Afrika. Wengine 11 bado wanaendelea kuwa huru na mahakama hiyo haina polisi yake yenyewe ya kuwakamata.