1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gbagbo ayanasa mabenki ya kigeni

19 Februari 2011

Nchini Cote d’Ivoire,rais anayewania muhula mwengine Laurent Gbagbo ameiagiza serikali yake kuchukua usimamizi kamili wa mabenki manne ya kigeni yanayoendesha shughuli zake nchini humo.

https://p.dw.com/p/10JRa
Rais Laurent Gbagbo wa Cote d'IvoirePicha: AP

Hatua hiyo inayagusa pia mabenki ya Citibank ya Marekani na Standard Chartered ya Uingereza.Mabenki hayo yaliyo na akaunti nyingi zaidi za wafanyakazi wa uuma,yalifungwa kwasababu ya vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi wa rais uliogubikwa na utata.Wakati huohuo,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema anaziunga mkono harakati za jopo maalum la marais wa Bara la Afrika wanaoushughulikia mzozo wa kisiasa wa Cote d'Ivoire.

Akaunti za umma

Rais anayeng'ang'ania kubakia madarakani Laurent Gbagbo ameiagiza serikali yake kuchukua usimamizi kamili wa mabenki mawili ya Ufaransa yaliyofungwa kwasababu ya ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa rais uliozua utata.Katika taarifa yake iliyosomwa na msemaji wake,Ahoua Don Mello,kwenye kituo cha taifa cha televisheni-usimamizi wa matawi ya mabenki ya BNP Paribas na Societe Generale ndio utakaobadilika.Kutokana na hali hiyo,watu kadhaa wanaripotiwa kuwa katika harakati za kuziondoa pesa zao kwenye mabenki hayo.Duru zinaeleza kuwa foleni nyingi za wateja zimeshuhudiwa nje ya afisi za mabenki hayo.

Ifahamike kuwa mabenki matano ya kigeni yalizifunga afisi na kusimamisha operesheni zake nchini Cote d'Ivoire,baada ya Benki Kuu ya eneo la Afrika Magharibi,BCEAO,kuyawekea vikwazo.Hali hiyo imesababisha uhaba mkubwa wa fedha kwenye mabenki hayo.Benki kuu ya BCEAO iliamua kuichukua hatua hiyo baada ya mgogoro wa kisiasa kutokea nchini humo kwasababu ya utata wa uchaguzi wa rais wa Novemba mwaka uliopita.Umoja wa Ulaya nao pia umemuwekea vikwazo vya usafiri Laurent Gbagbo na wapambe wake kama anavyoeleza Walter Linder,mwakilishi maalum wa Ujerumani katika masuala ya Afrika.

Elfenbeinküste UN Vertretung und Auto in Abidjan Flash-Galerie
Makao makuu ya Umoja wa Mataifa Cote d'Ivoire:wajibu wao ni kumlinda Ouatarra anayetambulika kimataifaPicha: DW

Msukumo na jopo

Ili kujaribu kuutafutia suluhu mkwamo huo,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amezipa msukumo mkubwa harakati za jopo maalum la marais wa bara la Afrika wanaoushughulikia mzozo huo wa Cote d'Ivoire.Kwenye taarifa yake,Ban Ki Moona aliwatolea wito washirika wote wa Cote d'Ivoire kushirikiana kikamilifu na jopo hilo la marais kwa mintarafu kuupatia suluhu mzozo huo wa kisiasa ulioikwamisha nchi. Ahmadou Toure ni msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Ivoire na anaeleza kuwa,"Ujumbe maalum wa wataalam walikuja hapa wiki iliyopita na wakafanya vikao na wawakilishi wa washirika muhimu.Walisharudi na tunaisubiri ripoti yao.Kikao cha kilele cha jopo la marais kimepangwa kufanyika tarehe 20 mwezi huu wa Februari.Sote tunasubiri,"alifafanua.

Elfenbeinküste Präsidentschaft
Guillaume Soro,Waziri mkuu wa Alassane OuatarraPicha: picture-alliance/dpa

Wiki ijayo

Jopo hilo la marais linasimamiwa na rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz na linawashirikisha pia marais Jacob Zuma wa Afrika Kusini,Idriss Deby wa Chad,Blaise Compaore wa Burkina Faso na Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE/UN

Mhariri:Miraji,Othman