1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GENEVA : Mkutano kulenga wakimbizi wa Iraq

17 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC9G

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa linaanza mkutano wa kimataifa wa siku mbili mjini Geneva kuelezea hali ya wakimbizi milioni nne wa Iraq.

Wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 60 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo ambao umepangwa kuanza leo hii.Mkutano huo utalenga mahitaji ya kibinaadamu kwa wakimbizi na watu waliopoteza makaazi yao nchini Iraq na katika nchi zilioko karibu na Iraq.

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linatumai mkutano huo utapelekea kuanzishwa kwa ushirika wa kimataifa kushughulikia tatizo hilo na kuhakikisha misaada kwa nchi jirani ambazo kwa kiasi kikubwa zimetwikwa mzigo huo.

Syria ina idadi kubwa kabisa ya wakimbizi hao ambao ni milioni 1.2,wakimbizi 750,000 wako nchini Jordan na zaidi ya 200,000 wako nchini Misri,Iran,Lebanone na Uturuki.

Takriban watu milioni 1.9 wamepotezewa makaazi ndani ya Iraq kwenyewe.