1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GENEVA:Msalaba mwekundu kuongeza misaada Afrika ya Kati

5 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBua

Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu limesema kuwa litaongeza misaada yake ya kibinaadamu katika Jamhuri ya afrika ya kati ambapo zaidi ya watu laki mbili na elfu 80 wanahitaji msaada kutokana na mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali.

Mkuu wa shirika hilo nchini humo, Jean-Nicolas Marti akizungumza mjini Bangui, amesema kuwa maelfu ya watu wanahitaji msaada kutokana na mapigano hayo.

Jamhuri ya afrika ya kati imeshuhudia miongo kadhaa ya vurugu yakiwemo mapinduzi na uasi toka ilipopata uhuru wake mwaka 1960.

Kwa sasa waasi wanaompinga Rais Francois Bozize wa nchi hiyo wanashikilia miji kadhaa iliyoko kaskazini.

Rais Francois Bozize aliingia madarakani kama muasi mwaka 2003, baada ya jeshi lake la uasi kumfurusha aliyekuwa rais Ange-Felix Patasse aliyekimbilia uhamishoni Togo.