1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Georgia yatangaza hali ya kivita

Nijimbere, Gregoire9 Agosti 2008

Rais wa Georgia, Mikhail Saakashwili ametangaza hali ya kivita kufuatia mapigano kati ya nchi yake na Russia katika jimbo la Ossasia ya kusini, linalopigania kujitenga na Georgia.

https://p.dw.com/p/EtaX
Rais wa Georgia, Mikhail SaakashwiliPicha: picture-alliance/ dpa

Bunge la Georgia limepitisha sheria ya hali ya kivita nchini kufuatia mapigano yanayopamba moto kati ya nchi yake na Russia katika jimbo la Ossasia ya kusini, linalopigania mjitengo na Georgia.

Hapo kabla, rais Mikhail Saakashwili, ametoa wito wa kusimamisha mapigano na kuituhumu kwa mara yningine tena Russia kuwa imeanza operesheni ya kijeshi kuivamia nchi yake. Rais Saakashwili amesema mashambulizi ya mabomu ya Russia kwenye vituo vya Georgia ni vitendo vya kigaidi. Mapigano hayo yalizuka wakati majeshi ya Georgia yalipolenga kuuteka mji mkuu wa jimbo la Ossasia ya kusini, Tskhinvali hapo jana. Waziri wa Russia wa mambo ya kigeni Sergei Lavrov, amesema watu wapatao 1,500 waliuawa katika mapigano hayo.

Wakati mapigano yakiendelea kati ya majeshi ya Georgia na Russia kulidhibiti jimbo la Ossasia ya kusini, balozi wa Marekani nchini Russia, Richard Holbrooke, ameivika lawama Russia kwamba inalenga kuuondoa utawala wa rais Mikhail Saakashwili.

Pande hizo mbili yaani Georgia na Russia kila moja anadai kuudhibiti mji mkuu wa Ossasia ya kusini Tskhinvali. Georgia imekuwa ikikusanya wanajeshi wake na imetangaza kuwa itawarejesha nyumbani wanajeshi wake 2,000 walioko Irak mnamo siku chache zijazo. Russia imesema hakutakuwepo na mazungumzo yoyote yale kabla ya majeshi ya Georgia kuihama Ossasia ya kusini.