Mgogoro wa Georgia
13 Agosti 2008Urusi na Georgia zimekubaliana na mpango uliopendekezwa na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa juu ya kutatua mgogoro baina yao nchi zao.
Lakini Urusi imesema,lazima Georgia iyarudishe majeshi yake yote kambini.
Rais Nicolas Sarkozy ambae kwa sasa ni rais wa Umoja wa Ulaya amefikia mapatano na Urusi na Georgia juu ya mpango wa kutatua mgogoro wa nchi hizo mbili baada ya vita vya siku tano.
Kwa mujibu wa mpango huo, Urusi na Georgia zitarudisha majeshi yao mahala yalipokuwapo kabla ya vita kuanza.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanajadili mpango huo mjini Brussels.
Hatahivyo Urusi imesema itaondoa majeshi yake kwenye ardhi ya Georgia ikiwa Georgia itayarudisha majashi yake kambini.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema hayo leo kwenye mkutano na wandishi habari mjini Moscow.
Ameeleza kuwa ikiwa majeshi ya Georgia yatarudishwa kambini, Urusi pia itayarudisha nyumbani majeshi yake yote kutoka Georgia.
Hatahivyo amesema kuwa walinda amani wa Urusi wataendelea kuwapo katika Ossetia ya kusini.
Katika hatua nyingine yenye lengo la kutatua mgogoro baina ya nchi yake na Urusi rais wa Georgia Saakashvili amesema sasa pana ulazima wa kupitishwa azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Baada ya mazungumzo yake na rais Dmitri Medvedev wa Urusi rais Nicolas Sarkozy alifahamisha mjini Moscow kuwa Urusi na Georgia zimekubaliana na mpango wa vipengee sita juu ya kuanza mazungumzo ya kuutatua mgogoro wa Georgia.
Lakini waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lawrov amesema itakuwa vigumu kwa nchi yake kufanya mazugumzo ya ana kwa ana na rais Saaka shvili.
Waziri huyo ameeleza kuwa rais huyo wa Georgia ametenda uhalifu dhidi ya watu wa Urusi bila ya kuifikiria madhara yake, na lingekuwa jambo bora iwapo angeliondoka.
Watu wapatao mia moja alfu wanakadiriwa kuwa wamepoteza makao yao kufuatia mapigano ya siku tano baina ya majeshi ya Uruis na ya Georgia.
Hatahivyo Urusi jana ilitangaza hatua ya kusimamisha mapigano baada ya kusema kuwa ilifikia shabaha yake. Wakati huo huo Urusi imefahamisha kuwa ilipoteza askari wake 74 katika mapambano na Georgia. Askari wake wengine 171 walijeruhiwa na 19 hawajulikani walipo.