1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana bila ya Essien itatamba Afrika Kusini?

7 Juni 2010

Ghana au Black Star, kama inavyojulikana inaelekea Afrika Kusini, bila ya jogoo wake Michael Essien, ambaye ameshindwa kupona majeraha yake ya goti.

https://p.dw.com/p/Njlw
Michael EssienPicha: AP

Hata hivyo kocha wa timu hiyo Milovan Rajevac ana matumaini ya kufanya vyema kwa timu yake.

Mwishoni mwa wiki Ghana ilimaliza mawindo yake kwa kuichapa Latvia bao 1-0 huko Milton Keynes Uingereza, ambapo kocha huyo alisema kuwa sasa kila kitu kiko barabara, na hakuna majeruhi yoyote.

Mapema kulikuwa na shakashaka kwa kiungo wake imara Sulley Muntari kutokana na maumivu ya paja, lakini pamoja na kushindwa kucheza katika mechi dhidi ya Latvia, lakini anatarajiwa kuvaa njumu katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Serbia.

Ghana imepangwa kundi moja na Ujerumani pamoja na Australia.Timu hiyo katika fainali zilizopita nchini Ujerumani mwaka 2006, ilionesha kandanda la kuvutia, ambapo ilikuwa timu pekee kutoka Afrika iliyofika raundi ya pili ilipotolewa na Italia iliyokuja kutwaa ubingwa.

Kikosi chake ndiyo kilikuwa na vijana wadogo zaidi kuliko timu nyingine wenye wastani wa umri wa miaka 23 na siku 352.Mara baada ya fainali hizo, shirikisho la kabumbu duniani FIFA liliiweka katika nafasi ya13 ya timu bora duniani.

Katika fainali za mwaka huu, Ghana pia ndiyo timu yenye wastani wa wachezaji vijana zaidi wakiwa na wastani wa aumri wa miaka 24 na miezi 9, ikifuatiwa na Korea Kaskazini.Brazil ndiyo timu yenye ´vijeba´ wengi yaani wachezaji wenye umri mkubwa wakiwa na wastani wa miaka 29 na miezi minne wakifuatiwa na Uingereza wenye umri wa miaka 29 na miezi miwili.

Hata hivyo, washabiki wengi nchini Ghana wana wasi wasi na timu yao kutokana na mfumo wa uchezaji ambao kocha Milovan anautumia,mtindo wa kuwa na mshambuliaji mmoja tu mbele.

Nahodha wa zamani wa timu hiyo ya Ghana Charles Akunnor, ni miongoni mwa wale wanaotiwa shaka na mfumo huo.Anasema kuwa Ghana kawaida yake huwa na washambuliaji wawili mbele yaani mfumo wao ni 4-4-2.

Kocha huyo Milovan humuweka mshambuliaji mmoja mbele Asamoah Gyan anayechezea Rennes ya Ufaransa .Lakini washabiki wa Ghana wanataka kuwe na washambuliaji wawili, Gyan na Prince Tagoe anayechezea klabu ya Hoffeinheim ya Ujerumani.

Katika nafasi ya kiungo Ghana inajivunia Stephen Apiyah anayechezea Bologna ya Italia, Sulley Muntari wa mabingwa wa Ulaya Inter Milan, pamoja na Kevin-Prince Boateng mzaliwa wa Ujerumani anayechezea Portsmouth ya Uingereza.Boateng ndiye aliyewatia majonzi wajerumani kwa kumuumiza nahodha wao Michael Ballack.

Ballack aliumizwa na Boateng katika fainali ya kombe la FA la Uingereza kati ya Chelsea na Portsmouth.Mdogo wake Jerome Boateng yumo katika kikosi cha Ujerumani.

Wachezaji hao ni wazaliwa wa Ujerumani kwa baba Mghana na mama mjerumani.Kaka mtu amechagua kuchezea Ghana na mdogo kaamua kuchezea Ujerumani, na iwapo watapangwa timu hizo zitakapokutana, itakuwa mara ya kwanza katika historia ya kombe hilo, kwa wachezaji ndugu kuchezea timu mbili tofauti.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/Reuters/Ghana Football Association

Mhariri:Josephat Charo