1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana na Morocco uwanjani leo

28 Januari 2008

Wenyeji Ghana wahitaji pointi 1 leo kukata tiketi ya robo-finali.Morocco lazima ishinde.

https://p.dw.com/p/CymK

Wenyeji Ghana, wanaohitaji sare leo,wanaingia uwanjani jioni hii mjini Accra wakitumai kuipiga kumbo Morocco na kuparamia kileleni mwa kundi A. Morocco lazima ishinde ili kuepuka kurudu Rabat. Kocha wa Senegal, Henri Kaspercza afunga virago baada ya Angola jana kuichezesha simba wa terange kindumbwe-ndumbwe na kuwazaba mabao 3:1.

Na Samuel Eto wa Kameroun,analenga kuivunja rekodi ya Muivory Coast Laurtent Pokou ya mabao 14 katika Kombe la Afrika.

Wenyeji Ghana wanaingia uwanjani hivi punde mjini Accra kwa mpambano na simba wa Atlas-Morocco wakiwa na shabaha alao kuondoka na pointi 1 ili kuingia duru ijayo.Wakishindas leo Black Stars na kutoroka na pointi 3 ,basi wataweza kuwaepuka tembo wa Corte d’Iviore duru ijayo ya robo-finali.

Simba wa atlas-morocco baada ya kuanza kwa vishindo walipoizaba Namibia mabao 5-1 kabla kutandikwa binafsi mabao 3-2 na Guinea,lazima leo wawashinde wenyeji ghana ili wakate tiketi yao ya robo-finali la si hivyo, simba wa Atlas wako njiani kufuata nyayo ya simba wa terange-Senegal waliokiona jana cha mtema kuni kutoka kwa paa wa Angola.

Guinea na Morocco kila moja ina pointi 3 ,lakini Guinea yadhihirika ina kibarua hafifu kuliko Morocco ikiwa na miadi na Namibia pia wakati mmoja na mpambano wa Morocco na Ghana .

Katika changamoto hii ya leo, Ghana itabidi ifanye mageuzi kati ya uwanja ,kwavile stadi wao wa kiungo Laryea Kingston hataweza kucheza leo kwa kufungiwa kucheza.

Morocco inatumai simba wa Atlas kutiwa shime na harufu nzuri ya mshambulizi wao Alloudi ambae aliumia baada ya kutia mabao 3 katika wavu wa Namibia.

Katika zahama kati ya Guinea na Namibia, Guinea itabidi kucheza bila ya Pascal Feindouno aliefungiwa kwa mechi 2 ,hatahivyo, Guinea yatazamiwa kufua dafu mbele ya Namibia.Kwani, namibia kama jirani zao Bafana Bafana wamo kufunga virago kurudi kusini mwa Afrika na kuwaachia wenzao Angola kuendelea kutamba katika kombe hili la Afrika.Mpambano wa leo kwa Namibia ni wa kuaga tu mashindano kwa heshima.

Kwa ufupi, Angola na Tunisia zimepungiwa na pointi 1 tu kuingia duru ijayo ya robo-finali.Angola na Tunisia zinakumbana alhamisi hii ijayo mjini Temale na kila moja itahitaji sare tu ili kuzitoa timu 2 nyengine katika kundi lao.

Mshambulizi Manucho anaejiunga na manchester united alipachika jana mabao 2 na mtunesia wa asili ya Brazil dos Santos akauona pia mara 2 mlango wa Bafana Bafana .

Kusema kweli, Angola iliwaambia simba wa Terange-Senegal kwamba „kutangulia-si kufika“.

Baada ya bao la kichwa la msenegal Abdoulaye Faye lililolifumania lango la Angola, Manucho alisawazisha.

Kwa pigo la jana la mabao 3-1, kocha wa Senegal, mpoland Henri Kasperczak ameamua kufunga virago na kujiuzulu.Kwani pigo la jana, limeichimbia kaburu Senegal hataikishinda mpambano ujao na Afrika Kusini.

Muivory Coast Laurent Poku,ambae rekodi yake ya mabao 14 katika kombe la Afrika ilisawazishwa jumamosi na simba wa nyika Samuel Eto’o,amesema haoni aibu kwa rekodi yake hiyo kukaribia kuvunjwa.Imedumu rekodi hiyo miaka 40,kitu ambacho si kibaya.“namtamkia kwahivyo, eto’o furaha nyingi.“

Ingawa anamuangalia samuel eto’o wa Kamerun ni mshambulizi hatari sana ,anaamini Pokou nahodha wa timu yake ya Cort d’Iviore Didier Drogba ni wa hadhiya juu zaidi kuliko mchezaji yeyote mwengine.Ni mchezaji alieumia,lakini alitaka kujiunga pamoja na timu yake katika kombe hili la Afrika.yeye ni mfano mwema.Samuel Eto’o alitia bao lake la 14 kusawazisha rekodi ya Laurent Pokou kupitia mkwaju wa penalty pale simba wa nyika waliponguruma kwa mabao 5-1 mbnele ya chipolopolo-Zambia.

Pokou alianza maisha yake ya dimba kama stadi wa kulipwa na klabu ya ASEX Mimosas mjini Abidjan.Baadae akaenda Ufaransa alimkoichezea Stade Rennes kati ya 1964-76 na 1978-90.halafu akajiunga na Nancy kati ya 1976 na 1978.

Kinyan’ganyiro cha kombe la Afrika la mataifa kiendelea hadi finali Februari 10, shirikisho la dimba la afrika-CAF lilihakikisha jana kwamba linazitia sana maanani taarifa za majaribio ya kulishia baadhi ya timu hongo kuleta mizengwe katika matokeo.Kwanza ilikua kocha wa Benin,mjerumani Reinhard Farbisch halafu ikawa Namibia kutoa mashtaka kwamba timu zao zilitakiwa kuachia magoli.Wakati benin ilitongozwa kwa kitita cha dala 20,000, Namibia iliambiwa ingechota dala 30.000 ikiwa itashindwa mpambano wake wa leo na Guinea.

Namibia ambayo haina nafasi ya ushindi leo dhidi ya Guinea ilimuarifu rais wa shirikisho la mpira la Namibia John Muinjo na yeye hakukawia kuiarifu CAF-shirikisho la dimba la Afrika.Mtu mmoja anaetumikia kituo cha kamari huko Asia, asemekana amehusika na mkasa huu wa kununua matokeo katika kombe la Afrika.Hadi sasa hakufanikiwa au ?

Kocha wa benin,mjerumani Rheinhard Farbisch ambae aliwahi kuwa kocha wa Kenya na Zimbabwe na hapo kabla alikuwa 1969 -1971 Borussia Dortmund, aliwaambia waandishi habari:

Niko tayari ikibidi hata kisheria kuthibitisha mashtaka niliotoa.“

Kombe la Afrika linaangaliwa vipi Afrika Mashariki huku kenya ikiendelea kuwa katika machafuko na Harambee Stars (Kenya) na Taifa Stars,Tanzania hazimo katika kombe hili.Je, Tanzania iliokua kundi moja na Senegal imejifunza nini kwa mchezo wa Angola jana ?

Mwishoe, riadha:

Msichana wa thiopia Meseret Defar,ameivunja j mwishoni mwa wiki rekodi ya dunia ya wanawake ya ukumbini-indoor ya masafa ya maili 2 huko Boston,Marekani.Bingwa huyo wa olimpik wa mita 5000,alichukua muda wa dakika 9 na na sekunde 10.50.