1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana na Senegal nani mbabe?

19 Januari 2015

Fainali za kombe la mataifa ya Afrika, AFCON, zinazofanyika nchini Guinea ya Ikweta, zinaingia katika siku ya tatu leo(19.01.2015),ambapo Ghana na Senegal zinapambana katika kundi C mjini Mongomo.

https://p.dw.com/p/1EMp8
Africa Cup of Nations 2014 - Senegal vs. Ägypten
Kikosi cha timu ya taifa ya SenegalPicha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Fainali za kombe la mataifa ya Afrika zinaingia katika siku yake ya tatu leo jioni, ambapo miamba ya soka barani Afrika Ghana na Senegal zinatiana kifuani wakianza kampeni ya kulinyakua taji hilo katika bara la Afrika.

Kundi hili na C linaonekana kuwa kundi gumu kabisa katika michuano hii, ambapo linajumuisha pia timu za Algeria na Afrika kusini ambazo zitaingia uwanjani usiku wa leo kuamua nani mbabe.

Africa Cup of Nations 2013
Kombe la mataifa ya AfrikaPicha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Nimezungumza na mchambuzi wa michezo kutoka Tanzania, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa na Pamba ya Mwanza khalid Bitebo ambaye anatathmini michezo minne ya mwanzo katika kinyang'anyiro hiki.

Tembo wa Cote D'Ivoire wataanza kampeni yao kwa mara nyingine tena kuwania kulinyakua kombe la mataifa ya Afrika kesho Jumanne wakati watakapooneshana kazi na majirani zao Guinea katika kundi D mjini Malabo kabla ya Cameroon na Mali kuingia dimbani kuonesha uwezo wao.

Tembo hao wa Cote D'Ivoire hawajashinda taji hilo tangu mwaka 1992, licha ya kuwa wamepata vipigo vya kuhuzunisha kwa mikwaju ya penalti katika mwaka 2006 na 2012 katika fainali, ambapo mara ya mwisho madhara yalifanywa na kikosi cha Herve Renard cha Zambia , Chipolopolo.

Na ni kocha huyo Mfaransa ambaye ana kazi ya kukiongoza kikosi cha Tembo hao kuweza kupata mafanikio hivi sasa nchini Guinea ya Ikweta.

Kikosi chake hakijaonesha uwezo mkubwa katika michuano ya kufuzu kucheza katika fainali, kikiambulia nafasi ya pili nyuma ya Cameroon , na Renard amedai kwamba kikosi chake hakiwezi kutambuliwa kama moja ya timu zinazoweza kutoroka na taji hilo, katika fainali hizi za 30 za kombe la mataifa ya Afrika , hususan tangu pale Didier Drogba alipoamua kutundika madaluga yake juu kwa timu ya taifa.

Interaktiver WM-Check 2014 Mannschaft Elfenbeinküste
Kikosi cha timu ya taifa ya Cote D'IvoirePicha: picture alliance/abaca

Pamoja na hayo Tembo wa Cote D'Ivoire bila shaka wana kikosi imara kabisa katika mashindano hayo, kikiwa na machezaji kama Serge Aurier , Kolo Ture, Gervinho, Seydou Doumbia na Wilfred Bony. na kisha kuna Yaya Toure, ambaye ni mchezaji bora wa mwaka katika bara la Afrika.

Simba wa Nyika Cameroon

Kikosi cha kocha Volker Finke Simba wa Nyika Cameroon kimefanikiwa kuondoa jinamizi la fainali za kombe la dunia nchini Brazil na kustaafu kwa nahodha Samuel Eto'o, kunatia shauku ya kufanya vizuri na kurejea nyumbani Yaounde na taji hilo.

Didier Drogba Fußballspieler Archivbild 2007
Didier Drogba mchezaji wa Cote D'Ivoire aliyestaafuPicha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

hata hivyo , hawatakuwa na huduma ya mchezaji wa kati na nahodha Stephane Mbia , ambaye anapata nafuu kutokana na maumivu aliyoyapata akicheza na timu yake ya Sevilla mapema mwezi huu lakini pia anatumikia adhabu ya kati nyekundu baada ya kutolewa nje akicheza dhidi ya Cote D'Ivoire mwezi Novemba mwaka jana.

Na katika kombe la mataifa ya bara la Asia mashindano yanayofanyika nchini Australia Iran ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, katika mchezo wa kundi C leo, ikiwa na maana kwamba wamewakwepa mabingwa watetezi Japan katika robo fainali.

UAE itapambana kwa hiyo na mshindi wa kundi D, huenda Japan katika robo fainali wakati Iran huenda ikapambana na Iraq. Japan inapambana na Jordan kesho katika mchezo wa mwisho wa kundi D ikiwania kushinda licha ya kuhitaji sare tu dhidi ya Jordan kuweza kushika nafasi ya kwanza katika kundi hilo.

Fußballer Diego Costa und Eden Hazard (FC Chelsea)
Wachezaji wa Chelsea LondonPicha: picture-alliance/dpa/F. Arrizabalaga

Mgombea wa FiFIA Jerome Champagne

Mgombea wa kiti cha urais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Jerome Champagne hajapata barua tano za kumuunga mkono kutoka katika vyama vya soka vya mataifa wakati muda wa mwisho wa uteuzi kukubalika kugombea umebakia siku kumi tu, amesema mgombea huyo raia wa Ufaransa leo.

Champagne, mwenye umri wa miaka 56 ambaye ni naibu katibu mkuu wa zamani wa FIFA, ambaye alizindua kampeni yake mjini London mwaka mmoja uliopita wiki kama ya leo, ametuma barua ya wazi kwa viongozi wa vyama 209 wanachama wa FIFA akiomba uungwaji mkono kabla ya tarehe 29 Januari ambayo ndio siku ya mwisho.

Ligi ya Uingereza Chelsea kidedea

Na katika ligi ya Uingereza kocha wa Chelsea Jose Mourinho ameueleza ushindi wa timu yake wa mabao 5-0 dhidi ya Swansea City kuwa na uchezaji uliokamilika, na wikiendi yake imemalizika vizuri jana Jumapili kwa Manchester City kupokea kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Arsenal London na kufungua mwanya wa pointi tano mbele ya Man City.

Campions League Schalke 04 gegen FC Chelsea
Jose Mourinho wa ChelseaPicha: picture-alliance/dpa

Arsenal ilionesha uwezo mkubwa jana katika msimu huu na kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Manchester City. Manchester United ilifanikiwa kuiangusha Queens Park Rangers kwa mabao 2-0.

Real Madrid ilijihakikishia nafasi ya juu katika ligi ya Uhispania La Liga kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Getafe na jana Jumapili Lionel Messi alipachika mabao 3 na kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Deportivo la Coruna.

Na nchini Italia Carlos Tevez alipachika ambao 2 katika ushindi wa Juventus Turin wa mabao 4-0 dhidi ya Helass Verona jana Jumapili, wakati SSC Napoli ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Roma. Napoli ina point 33 , mbili nyuma ya Lazio Roma ikiwa katika nafasi ya nne na nafasi ya kucheza katika Champions League.

Wakati huo huo Chelsea inakabana koo kesho(20.01.2015) na Liverpool katika nusu fainali ya kombe la FA. Na siku ya Jumatano Tottenham Hotspur ina miadi na Sheffield United.

Wakati ligi ya Ujerumani Bundesliga ikiwa bado katika mapumziko, Borussia Dortmund ambayo imeanza msimu huu kwa kusua sua ikiwa katika nafasi ya 17 katika ligi yenye timu 18 bado inaandamwa na majeruhi ambapo katika michezo ya kujiandaa na ligi mchezaji wa kati Sebastian Kihl na Kevin Grosskreutz wameumia katika siku ya mwisho ya kambi ya mazowezi nchini Uhispania, klabu hiyo imesema leo.

Dortmund mabingwa wa Bundesliga mwaka 2011 na 2012 wako nafasi ya 17 wakati michuano hiyo ikirejea dimbani mnamo Januari 30 baada ya mapumziko ya majira ya baridi.

Timu hiyo imekuwa ikiandamwa na majeruhi msimu huu, wakimkosa mshambuliaji Marco Reus kwa miezi kadhaa pamoja na Ilkay Gundorgan , Jakub Blaszczykowski, Socratis Papastathopoulos, Nuri Sahin na Marcel Schmelzer miongoni mwa wengine wengi.

Dortmund itakabiliana na Juventus katika kinyang'anyiro cha Champions League

Tennis.

Rafael Nadal amefanikiwa kumshinda Mikhail Youzhny wa Urusi mwanzoni mwa mashindano ya Australian Open leo na kuvuka kikwazo cha kwanza katika michuano hiyo. Roger Federer, akifukuzia ubingwa wake wa tano wa taji hilo la Australian Open anatarajiwa kupambana na Lu Yen-Hsun wa Taipei leo.

Kwa taarifa hiyo ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo jioni ya leo, hadi mara nyingine kwaherini.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / ape

Mhariri: Josephat Charo.