1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana Uchaguzi- Atta Mills anaongoza katika matokeo ya mapema

Eric Kalume Ponda29 Desemba 2008

Matokeo ya mapema nchini Ghana, yanaonyesha kiongozi wa upinzani Atta Mills anaongoza dhidi ya Nana Akufo Addo.

https://p.dw.com/p/GOsy
Wafuasi wa chama cha upinzani cha National Democratic Congress NDC kinachoongozwa na Atta MillsPicha: AP


Kiongozi wa chama cha upinzani cha National Democratic Congress NDC, Atta Mills anaongoza dhidi ya mgombea wa chama tawala cha New Patriotic NPP Nana Akufo Addo.


Chama cha upinzani cha National Democratic NDC kilishinda duru ya kwanza ya uchaguzi huo uliofanyika tarehe 7 mwezi huu, ingawa hakikupata ushindi wa moja kwa moja kukiwezesha kuunda serikali.


Licha ya pande hizo mbili kulaumiana kuhusu vitisho na dosari vilivyoshuhudiwa wakati wa zoezi zima la uchaguzi,uchaguzi huo hata hivyo umechukuliwa kuwa mtihani mkubwa kwa demokrasia kote Barani Africa.


Kwa mujibu wa ripoti ya hivi punde kuhusu matokeo ya kura zilizohesabiwa kutoka maeneo bunge 187 kati ya 230, mgombea huyo wa chama cha National Democratic, Atta Mills alikuwa akiongoza kwa asilimia 51.7 dhidi ya mpinzani wake Akufo Addo aliye na asilimia 48.2.


Wakati wa duru ya kwanza ya Uchaguzi nchini humo, kiongozi huyo wa upinzani alishinda kwa jumla ya viti 114 dhidi ya viti 107 vilivyonyakuliwa na chama tawala cha NPP

katika bunge hilo lenye viti 230.


Tume ya uchaguzi nchini humo inasema kuwa tayari imethibitisha matokeo ya kura zilizohesabiwa katika maeneo bunge 38, ambayo pia yanamweka mbele Atta Mills, dhidi ya mpizani wake, huku matokeo kamili ya uchaguzi huo yanapotarajiwa siku ya jumanne.

Wagombea hao wawili wamekuwa wakilaumiwana kwa kuhusika na vitisho wakati wa uchaguzi, huku muungano wa mashirika ya wachunguzi wa kigeni na wale wa kutoka nchini humo, ukidai kuwa uchaguzi huo umekumbwa na dosari nyingi zaidi ikilinganishwa na duru ya kwanza.


Mashirika hayo yanasema kuwa yatanzisha uchunguzi kuhusiana na madai hayo.

Hata hivyo mjumbe maalum wa Marekani kwenye uchaguzi huo, ambaye ni naibu wa waziri wa mambo ya nje anayehusika na masuala ya Africa nchini Marekani,Jendayi Frazer, alionya kuwa matamshi ya viongozi hao wawili ni hatari, na yanayoweza kubadili hali ya utulivu wa kisiasa nchini humo.


Frazer alitaja madai hayo kuwa uvumi ambao hauwezi kuthibitishwa, na kwamba vyama hivyo viwili vya kisiasa vinajaribu kupandisha hisia za wapiga kura kabla ya uchaguzi kukamilika.


Mjumbe huyo aliongeza kusema kuwa uchaguzi wa Ghana sio tu fursa ya utawala wa kidemokrasia wa kupokezana madaraka baada ya rais aliyepo madarakani kumaliza muda wake wa kuhudumu, bali mtihani mkubwa kwa viongozi kote barani Africa.


Huu ni uchaguzi wa tatu kuandaliwa nchini Ghana tangu taifa hilo kuanza kuzingatia mfumo wa demokrasia mwaka wa 1992.


Mataifa mengi barsani Africa yamekumbwa na Ghasia za uchaguzi na kusababisha watu wengi wasio na hatia kuuawa.


Ni wiki iliyopita tu ambapo taifa jirani la Guinea lilikumbwa na mapinduzi ya umwagikaji damu masaa machache tu baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Lansana Conte.


Kadhalika mnamo mwezi Agosti mwaka huu mapinduzi yaliyotokea nchini Mauritania yalimuondoa madarakani kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo.