1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana Uchaguzi- Rais mteule Atta Mills anendelea kupongezwa.

Eric Kalume Ponda5 Januari 2009

Jamii ya Kimataifa inaendelea kumpongeza rais mteule nchini Ghana John Atta Mills kufatia ushindi wake wa siku ya Jumamosi.

https://p.dw.com/p/GSE1
Rais mteule nchini Ghana John Atta Mills ajiandaa kuliongoza taifa hilo kufuatia ushindi wake siku ya JumamosiPicha: AP


Huku pazia la uchaugi nchini humo linapofungwa na rais huyo mteule anapojiandaa kuingia madarakani hapo Januari 7, jamii ya kimataifa imetaja kuwa kielelezo cha demokrasia barani Africa.


John Atta Mills wa chama cha National Democratic Congress NDC, alitangazwa mshindi dhidi ya mpinzani wake kiongozi wa chama tawala cha New Patriotic NPP, Nana Akufour Addo.


Baada ya kiongozi huyo wa chama cha upinzani kutangazwa mshindi siku ya Jumamosi, wakaazi wa taifa hilo sasa wameanza kurejea katika maisha ya shughuli zao za kawaida kufuatia hofu iliyokuwepo kwamba huenda uchaguzi huo ungekumbwa na ghasia.


Rais huyo mteule John Atta Mills aliwaomba wakaazi wa taifa hilo kuunga mkono serikali yake ili taifa hilo liwe mfano wa kukomaa kwa demokrasia barani Africa.


John Atta Mills alimshinda mpinzani wake Nana Akufour Addo kwa wingi wa kura 40,000 kati ya jumla ya kura millioni 9 zilizopigwa wakati wa uchaguzi huo ulioingia duru ya pili mwishoni mwa wiki iliyopita, katika eneo bunge la Tain,ambalo halikuweza kushiriki zoezi hilo Jumapili ya wiki iliyopita, kutokana na kasoro katika usafirishaji wa makaratasi ya kura katika eneo hilo.


Atta Mills sasa anachukua mahala kwa rais anayeondoka madarakani John Kufour ambaye ameliongoza taifa hilo kwa miaka minane ya vipindi viwili. Tayari rais huyo mteule ametangaza kamati yake itakayoshughulikia shughuli ya upokezanaji madaraka, baada ya ushindi kwenye uchaguzi huo ambao ni wa tano kuandaliwa kidemokrasia nchini humo tangu mwaka wa 1992.

Hata hivyo kiongozi wa chama cha New Patriotic Nana Akufour Addo, yaripotiwa ametangaza kwamba atakwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo akitaja vitisho na visa vya udanganyifu vilivyotelekelezwa na chama cha NDC hasa katika maeneo yenye ufuasi mkubwa.


Tangazo hilo hata hivyo linaonekana kupingwa vikali na rais anayeondoka madarakano John Kufour, ambaye amemtaka Nana Akufour Addo kuheshimu matokeo ya uchaguzi huo na kukubali kushindwa.


Katibu mkuu wa umoja wa Matifa Ban Ki-Moon amepongeza uchaguzi huo wa Ghana, akuitaja kuwa kioo na mfano wa kuigwa barani Africa, ambamo mataifa mengi yametumbukia katika ghasia za umwagikaji wa damu baada ya uchaguzi.


Waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga pia amempongeza Rais huyo mteule, akisema kuwa uchaguzi huo ni mfano wa pekee barani Africa.


Zaidi ya watu 1,000 walifariki nchini Kenya mwanzoni mwa mwaka uliopita kufuatia ghasia za uchaguzi, baada ya waziri mkuu Raila Odinga kumshtumu Rais Mwai Kibaki kwa kuiba kura.


Hali kadhalika Zimbabwe bado inakabiliwa na hali ngumu ya kisiasa kufuatia migogoro wa kiaisa baina ya chama cha upinzani kinachoongozwa na Morga Tschangirai, na rais Robert Mugabe ambaye amekatilia madarakani licha ya kushindwa wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi huo mwezi machi mwaka uliopita.

Kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Mauritania alipinduliwa mwezi Agosti mwaka uliopita hali ambayo pia imelitumbukiza taifa hilo katika kiza cha demokrasia. Hali kama hiyo pia imetokea nchin i Guinea ambako jeshi lilichukua utawala kufuatia kifo cha rais wa nchi hiyo Lansana Conte.


Baada ya kukamilika kwa uchaguzi nchini Ghana, sasa macho yanaelekezwa nchini Africa Kusini ambayo migogoro ya kisasa miongoni mwa viongozi wa chama tawala cha African Nationa Congress ANC, imezua mgawanyiko mkubwa huku taifa hilo linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.


Rais Kgalema Motlanthe ameupongeza uchaguzi wa Ghana akiosema kuwa ni dhihirisho la kuheshimiwa kwa demokrasia.