1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia baina ya waandamanaji na maafisa wa polisi zazuka Tunisia

28 Oktoba 2011

Huku chama cha kiislamu cha Ennahda kikichukua ushindi kufuatia uchaguzi wa kihistoria Tunisia, sasa makabiliano makali yamezuka kati ya waandamanaji na maafisa wa polisi nchini humo.

https://p.dw.com/p/130wx
Waandamanaji TunisiaPicha: dapd

Chama cha kiislamu cha Ennahda ambacho kinaendelea na mikakati ya kuunda serikali ya mpito nchini humo, kimetangazwa kuchukua ushindi wa viti 90 kati ya 217 vya bunge litakalokuwa na kibarua cha kutunga katiba mpya, kuunda serikali ya mpito na kuandaa uchaguzi nchini Tunisia.

Huku chama hicho kikiendelea na mikakati hiyo, sasa ghasia zaidi zimeibuka kati ya waandamanaji na maafisa wa polisi katika mji wa Sidi Bouzid, mji ambao ni chimbuko la wimbi la mapinduzi ya raia katika nchi za kiarabu miezi tisa iliyopita, yaliomshinikiza rais wa zamani Zine El Abidin Ben Ali kuondoka madarakani na kukimbilia mafichoni nchini Saudi Arabia.

Waandamanaji hao walikuwa wakilalamika juu ya kuondolewa au kufutwa kwa viti vilivyoshindwa na chama chao kinachoongozwa na mfanyibiashara Hachmi Hamdi. Hata hivyo tume ya uchaguzi nchini humo inasema chama hicho kilikiuka sheria za uchaguzi.

Polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao waliochoma moto ofisi za meya mjini humo na pia ofisi za chama kinachoongoza cha Ennahda.

Kulingana na Hafed Abdulli aliyeshuhudia makabiliano hayo, bado waandamanaji waliendelea kuchoma matairi barabarani na kuzidisha ghasia zaidi. Chama hicho kiliibuka cha nne katika uchaguzi wa kihistoria uliofanyika nchini Tunisia, kabla ya ushindi wa viti vyake bungeni kufutiliwa mbali na tume ya uchaguzi. 

Tunesien Wahlen
Rashed Gannouchi kiongozi wa EnnahdaPicha: DW

Huku hayo yakiarifiwa kiongozi wa chama cha Ennahda Rachid Ghannouchi amelaani vikali kitendo hicho na kusema bado wataendelea na mapinduzi hadi Tunisia iwe huru. " Tumewapa ahadi kuwa tutaendelea kuyadumisha mapinduzi katika Tunisia ilio huru, inayojitegemea, inayoendelea, yenye neema na ambayo haki za Mwenyezi Mungu, za mtume, za wanawake, za wanaume, za wenyedini na za waio na dini zitaheshimiwa, kwa sababu Tunisia ni ya kila mtu" Alisema Rashed Ghanouchi kiongozi wa chama cha Ennahda.

Sasa wanasiasa wasioegemea dini wanahofu kuwa chama cha kiislamu kitaweka sheria kali za kiislamu kwa jamii nchini humo, ingawa kiongozi wa chama Rashid Ghanouchi amepinga hilo. Maafisa wake wamesema hakutakuwa na vikwazo vyovyote kwa raia wa kigeni, unywaji wa pombe wala mavazi.

Mwandishi: Amina Abubakar/ AFPE

Mhariri: Josephat Charo