1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia mpya zasimamisha maisha Bujumbura

11 Desemba 2015

Milio mikubwa ya risasi na miripuko ya magruneti vimetikisa maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Burundi Bujumbura mapema Ijumaa, ambapo watu wanane wameripotiwa kuuawa.

https://p.dw.com/p/1HLl3
Burundi Soldaten Sicherheitskräfte Militär
Picha: picture-alliance/dpa/D. Kuroawa

Mshauri wa Rais nchini Burundi amesema wengi wa wavamizi waliovamia maeneo ya kambi za kijeshi mjini Bujumbura mapema siku ya Ijumaa wameua au kukamatwa.

Willy Nyamitwe ameandika kwenye mtandao wa twita kuwa "Hali inarejea kawaida huku silaha zikitwaliwa, wengi wa Sindumuja wameaua au kukamatwa".Sindumuja ni neno linalotumiwa kumaanisha wapinzani.

Shuhuda wa shirika la Reuters alisema milio ya risasi ilisikika mjini Bujumbura baada ya ujumbe huo kwenye mtandao wa twita.

Awali mwanajeshi mmoja alisema wanajeshi wawili na washambulizi watano waliuawa.

Kulingana na walioshuhudia kulikuwa na mapigano katika maeneo kadha yaliyo karibu yakiwemo Ngagara, Musaga, Nyakabiga na Kanyosha.Msemaji wa polisi Pierre Nkurikiye ameliambia shirika la habari la Ujerumani DPA kuwa "Wahalifu walivamia vijiji vya Musaga na maeneo ya Ngagara lakini polisi wanawasaka. "Tumeomba raia kusalia majumbani mwao kwa sababu za kiusalama", alisema Nkurikiye.

Msemaji wa serikali ya Burundi, Willy Nyamitwe
Msemaji wa serikali ya Burundi, Willy NyamitwePicha: DW/J. Johannsen

Kambi tatu za jeshi zashambuliwa

Walioshuhudia wamesema baadhi ya kambi za kijeshi zilivamiwa,huku wengine wakisema walisikia mizozano kati ya wanajeshi.Mapigano ya hivi karibuni yamekuwa kati ya wanaounga mkono upande wa serikali wakiwemo polisi na vijana wa chama kinachotawala kijulikanacho kama Imbonerakure wakipambana na makundi kadhaa yanayompinga Rais Pierre Nkurunziza.

Wengi wa waasi wanaopinga Nkurunziza wanasemekana kuwa waliacha kazi ya jeshi na kumuunga mkono Godefroid Niyombare,afisa wa jeshi la Burundi ambaye aliongoza jaribio la mapinduzi dhidi Nkurunziza mapema mwaka huu,kulingana mtu mmoja kutoka idara ya ujasusi ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Msemaji wa Rais Willy Nyamitwe alisema kupitia twita "Wakati waangalizi wa kimataifa wako nchini, kunatokea milio ya risasi usiku"

Amesema watu wenye silaha walijaribu kuvamia kambi za kijeshi usiku lakini wakashindwa.

Milio ya risasi karibu na gereza

Ujumbe mwingine wa twita ni kutoka kwa msemaji wa jeshi Gaspard Baratuza ambaye alisema milio ya risasi ilisikika karibu na gereza la Mpimba kwa nia ya kuachilia huru wafungwa lakini jaribio hilo halikufanikiwa.

Hali ya usalama nchini Burundi imeyumba baada ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu
Hali ya usalama nchini Burundi imeyumba baada ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatuPicha: picture-alliance/AP Photo

Kulingana na afisa mmoja mkuu wa jeshi ambaye hakutaka jina lake litajwe,mapigano yalianza mwendo wa saa kumi alfajiri wakati watu wenye silaha nzito walipovamia kambi ya jeshi ya Ngagara kaskazini ya mji wa Bujumbura na chuo cha mafunzo ya kijeshi eneo la kusini.

Afisa huyo alisema baada ya mapigano ya zaidi ya saa mbili jeshi lilizuia mashambulizi yaliyotokea kusini,huku wavamizi wengi wakiuawa katika kambi ya Ngagara. Amesema "wavamizi wengi wameuawa ingawa pia nasi pia tumepata hasara."

Burundi imekuwa ikikabiliwa na mapigano kati ya polisi na makundi yenye silaha tangu mwezi Aprili wakati Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kuwania muhula wa tatu mamlakani.Nkurunziza alishinda uchaguzi huo ambao ulisusiwa na upinzani mwezi Julai.

Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema zaidi ya watu 240 wameuawa kwenye maandamano hayo tangu mwezi Aprili,huku wengine 220,000 wanaaminika kuihama nchi hiyo. Muongo mmoja uliopita karibu watu 300,000 waliuawa kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi kati ya makundi ya kikabila ya Wahutu na Watusti.

Mwandishi:Bernard Maranga/Reuters/DPA/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga