1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia siku ya mwisho ya kampeni DRC

27 Novemba 2011

Siku ya mwisho ya kipindi cha kampeni ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeghubikwa na ghasia baina ya mgombea mkuu wa upinzani Etienne Tshisekedi na polisi hapo jumamosi.

https://p.dw.com/p/13HyR
Rais wa sasa na mgombea wa wadhifa huo, Joseph Kabila, wa Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo.Picha: AP

Polisi ilipiga marufuku shughuli za vyama vyote kuendelea na kampeni baada ya mtu mmoja kuuawa katika makabiliano kati ya wafuasi wa kambi tofauti za kisiasa.

Maelfu ya watu wanaomuunga mkono Etienne Tshisekedi walijipanga kwenye barabara kuu iendayo kwenye uwanja wa ndege katika kile walichosema ni kumpa kiongozi wao mapokezi sawa na yale aliyopata Yesu mjini Yerusalemu.

Mapokezi hayo lakini yalikuwa kinyume na marufuku iliyotangazwa na polisi kusimamisha shughuli zote za kampeni, baada ya mtafaruku wa jumamosi kusababisha kifo cha mtu mmoja, ambaye alipigwa na kipande kikubwa cha jiwe kichwani.

Bwana Tshisekedi alijitokeza akiwa kwenye gari kubwa aina ya Hummer yenye paa lililo wazi, lakini akazuiliwa na magari ya polisi yaliyoweka kizuizi barabarani. Kwa muda wa masaa matatu kiongozi huyo wa upinzani alikataa kuahirisha mkutano wake wa mwisho na wafuasi wake.

Gavana wa jimbo la Kinshasa Andre Kimbuta alisema shughuli za kumaliza kampeni zilipigwa marufuku kwa sababu za kiusalama, akiwashutumu wafuasi wa Tshisekedi kujihami kwa mapanga, visu na mabomu ya petroli.

Lakini Tshisekedi alisema gavana huyo anamwakilisha rais Joseph Kabila, na kuapa kuwa atakaidi amri zake. Msemaji wa Tshisekedi aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba mgombea wao aliombwa kuchagua kati ya mambo mawili; ama kuondoka kwenye uwanja wa ndege akisindikizwa na msafara wa polisi, au kubakia hapo hadi usiku wa manane.

Jibu la Tshisekedi kwa polisi likuwa ''Nitakutana na wafuasi wangu baada ya usiku wa manane''.

Vyama viwili vikubwa katika uchaguzi wa mwaka huu, yaani kile cha rais wa sasa Joseph Kabila na cha mpinzani mkuu Etienne Tshisekedi vilitaka kufanya mikutano yao ya mwisho kwenye uwanja wa mashahidi, hali ambayo ilizusha hofu kubwa ya kutokea uhasama na fujo baina ya wafuasi wa vyama hivyo.

Wagombea urais wa vyama hivyo walitazamiwa kuwasili mjini Kinshasa kutokea mikoani. Wafuasi wa Etienne Tshisekedi waliuvurumshia mawe msafara wa magari yaliyokuwa yakienda kumpokea rais Kabila . Polisi walifyatua risasi kuwatawanya , na watu watatu walijeruhiwa katika purukushani hizo.

Umati wa watu ulipungua kutokana na mbinyo wa ploisi, lakini ukaongezeka tena pale mgombea wao Etienne Tshisekedi alipowasili kwa njia ya barabara, kufuatia agizo la mamlaka ya viwanja vya ndege kuiamuru ndege aliyokuwa akisafiria kutua kwenye uwanja mwingine mdogo.

Vurugu hizo ziliashiria mwisho wa kipindi cha kampeni kilichijaa vurugu na makabiliano kati ya wafuasi wa vyama vinavyokinzana. Kutokea kwa vurugu hizo kunatarajiwa kuchochea hisia kuwa uchaguzi hautakuwa huru.

Rais wa sasa Joseph Kabila aliyezaliwa upande wa mashariki ya nchi, na ambaye hajui vizuri lugha ya Lingala ambayo ndio huzungumzwa zaidi mjini Kinshasa, ana wafuasi wachache kwenye mji mkuu, lakini anao ufuasi mkubwa katika maeneo mengine ya nchi.

Sambamba na vurugu hizi kwenye siku ya mwisho ya shughuli za kampeni, tume ya taifa ya uchaguzi jana iliahirisha mara mbili mkutano na waandishi wa habari juu ya hatua iliyopigwa kwenye maandalizi ya uchaguzi. Lakini mwenyekiti wa Tume hiyo Daniel Ngoy Mulunda amesisitiza leo (Jumapili) kuwa uchaguzi utafanyika tarehe 28 Novemba kama ilivyopangwa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP
Mhariri:Saumu Mwasimba