1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia za kisiasa zaitingisha Bangkok

1 Desemba 2013

Polisi ya Thailand imetumia gesi ya kutowa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji Jumapili(01.12.2013) wakati walipokuwa wakijaribu kuvamia makao makuu ya serikali kumpinduwa Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra.

https://p.dw.com/p/1ARJ2
Maandamano ya kupinga serikali Bangkok (01.12.2013)
Maandamano ya kupinga serikali Bangkok (01.12.2013)Picha: Reuters

Ghasia hizo ni mfulululizo wa mfarakano wa kiraia katika nchi hiyo ya kifalme tokea magenarali wenye kuupendelea ufalme kumpinduwa tajiri mkubwa wa nchi hiyo aliekuja kuwa waziri mkuu Thaksin Shinawatra miaka saba iliopita.

Maandamano hayo ya mitaani yenye lengo la kuindowa serikali ya Yingluck na badala yake kuliweka "baraza la wananchi " lisilochaguliwa na wananchi ni maandamano makubwa kabisa ya umma kuwahi kushuhudiwa tokea maandamano ya kumuunga mkono Thaksin mjini Bangkok miaka mitatu iliopita kusababisha kuuwawa kwa watu chungu nzima kutokana na maandamano hayo kuvunjwa kwa nguvu na jeshi.

Polisi yatumia gesi ya machozi

Kwa mujibu wa polisi watu wanaokadiriwa kufikia 35,000 walishiriki maandamano ya upinzani Jumapili.Polisi mara kadhaa imetumia gesi ya kutowa machozi wakati waandamanaji vichwa mchungu walipokuwa wakijaribu kwa masaa kuvunja vizuizi na kukata senyen'ge zilizokuwa zimeyahami jengo la makao makuu ya serikali ambalo lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya usalama wakiwemo wanajeshi wasiokuwa na silaha.

Waziri Mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra.
Waziri Mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra.Picha: Reuters

Inaelezwa kwamba Yingluck alikuwa hayuko katika jengo hilo wakati huo na serikali imekanusha uvumi kwamba ameikimbia nchi hiyo lakini mahala aliko hakujulikani na hakuonekana hadharani. Awali ilirepotiwa kwamba waziri mkuu huyo ilibidi kuondolewa kwenye jengo moja la polisi wakati waandamanaji walipokuwa wakitaka kulivamia.

Gesi za kutowa machozi pia zimetumika dhidi ya waandamanaji karibu na makao makuu ya polisi ya jiji kilomita kadhaa kutoka makao makuu ya serikali.Wakati kiza kilipoingia waandamanaji wenye mitarimbo walionekana karibu na makao makuu hayo ya serikali.

Kiongozi wa upinzani ashutumiwa

Katika mkutano na waandishi wa habari ulioonyeshwa na televisheni naibu waziri mkuu Pracha Promnog ameshauri wananchi wabakie nyumbani kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi na moja alfajiri kwa usalama wao.Ameongeza kusema serikali inaidhibiti hali hiyo na itarududisha hali kuwa ya kawaida haraka iwezekanavyo

Amemshutumu kiongozi wa maandamano hayo Suthep Thaugsuban kwa kutaka kupinduwa makao makuu ya serikali jambo ambalo ni uhaini unaostahiki kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo.

Kiongozi wa maandamano ya upinzani na naibu waziri mkuu wa zamani Suthep Thaugsuban akiwa kwenye maandamano ya upinzani mjini Bangkok.
Kiongozi wa maandamano ya upinzani na naibu waziri mkuu wa zamani Suthep Thaugsuban akiwa kwenye maandamano ya upinzani mjini Bangkok.Picha: Reuters

Ghasia ziliibuka jana usiku katika eneo karibu na uwanja mmoja ulioko viungani ambapo maelfu ya wafuasi wa serikali wenye fulana nyekundu walikuwa wamekusanyika kumuunga mkono Yingluck ambaye amekuwa akikabiliwa na maandamano ya mitaani kwa wiki kadhaa.

Kwa mujibu wa kituo cha kushughulikia hali ya dharura mjini Bangkok cha Erawan watu wanne wameuwawa na wengine 57 wamejeruhiwa. Watu waliouwawa na wale waliojeruhiwa walikuwa na majeraha mbali mbali kuanzia ya risasi na hadi kuchomwa visu.Basi moja la ghorofa pia limetiwa moto Jumapili katika eneo hilo hilo la kiunga cha Ramkhamhaeng.

Kiongozi wa maandamano hayo ya kupinga serikali Suthep amewataka watumishi wote wa serikali kugoma hapo Jumatatu juu ya kwamba haiko wazi watu wangapi wataitikia wito wake huo ambao umekataliwa na serikali

Polisi wa Thailand mjini Bangkok.
Polisi wa Thailand mjini Bangkok.Picha: Reuters

Wanajeshi wamwagwa kuimarisha usalama

Wakati idadi ya waandamanaji imepunguwa sana tokea ilie iliokadiriwa kufikia 180,000 kujiunga na maandamano hayo ya upinzani hapo Novemba 24 wamekuwa wakizidi kuziandama taasisi muhimu za serikali kwa kile wataalamu wanachoamini kuwa kinaweza kuwa jaribio la kuchochea mapinduzi ya kijeshi.

Nchi hiyo ya kifalme imeshuhudia mapinduzi au majaribio ya mapinduzi 18 tokea mwaka 1932 la karibuni kabisa likiwa lile la kupinduliwa kwa Shinawatra hapo mwaka 2006 lakini inaonekana jeshi limekuwa likisita kuingilia kati mzozo huo uliopo hivi sasa.

Serikali imeweka zaidi ya wanajeshi 2,700 kuimarisha usalama mjini Bangkok ambapo ni mara ya kwanza kutumika kwa idadi kubwa ya wanajeshi kukabiliana na machafuko.

Waziri Mkuu wa zamani wa Thailand Thaksin Shinawatra.
Waziri Mkuu wa zamani wa Thailand Thaksin Shinawatra.Picha: picture-alliance/dpa

Maandamano hayo yamechochewa na muswada wa msamaha ambao sasa umetelekezwa na chama tawala na ambao wapinzani walihofu ungeliruhusu kurudi kwa Thaksin anayeishi uhamishoni ambaye kupinduliwa kwake na magenerali wanaounga mkono ufalme kuliibuwa machafuko ya kisiasa yaliodumu kwa miaka kadhaa.

Thaksin anapendwa na watu wengi walioko vijijini na tabaka la wafanyakazi kutokana na sera zake za kujali wananchi wakati alipokuwa madarakani lakini anachukiwa na watu wengi walioko kusini mwa nchi hiyo,Wathailand wa tabaka la kati na vigogo vya Bangkok ambao wanamuona kwa ni mtu aliyetopea rushwa na ni tishio kwa ufalme wa nchi hiyo.

Vyama vinavyomuunga mkono Thaksin vimekuwa vikishinda kila uchaguzi kwa zaidi ya muongo mmoja lakini Yingluck hakuonesha ishara kwamba anafikiria kuitisha uchaguzi mpya kama njia ya kuondokana na mzozo huo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Abdu Mtullya