1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DW inafanya kongamano kubwa la vyombo vya habari

25 Juni 2015
https://p.dw.com/p/1Fkfp
GMF 2015 Eröffnung Peter Limbourg
Picha: DW/M. Magunia

Rais wa Marekani Barack Obama anapoandika ujumbe mfupi kwenye mtandao wa Twitter, ujumbe huo unawafikia watu wapatao milioni 60 duniani kote. Obama ndiye mwanasiasa mwenye wafuasi wengi zaidi katika Twitter. Kwenye orodha ya watu maarufu wenye wafuasi wengi anafuatia mkuu wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis, namba tatu ni rais wa India, Narendra Modi.

Mtandao wa internet pamoja na mitandao ya kijamii imekuwa vyombo vya muhimu kabisa katika kueneza siasa na diplomasia. Leo hii viongozi wa nchi 170 wana akaunti kwenye mtandao wa Twitter. Kwa hakika, mapinduzi ya dijitali sasa yameingia mpaka kwenye viwanja vya siasa. Uhusiano kati ya vyombo vya habari na siasa za mambo ya nje ndio mada kuu itakayoongoza kongamano la nane la Deutsche Welle linalofahamika kama Global Media Forum. Washiriki wapatao 2,000 kutoka nchi 130 watafika Bonn kwa ajili ya siku tatu za warsha, midahalo na hotuba. Miongoni mwao wamo waandishi wa habari 500.

Je, ni namna gani matumizi ya mtandao kwa ajili ya kusambaza propaganda za itikadi kali yataweza kuzuiwa? Hiyo ni moja ya mada watakayojadili washiriki wa kongamano. Watazungumzia pia namna ripoti kuhusu migogoro zinavyoweza kuathiri migogoro yenyewe. Kwa mfano, namna ambavyo mgogoro unaoendelea Ukraine hauendeshwi kwa silaha tu bali umegeuka kuwa vita vya taarifa na propaganda.

Ralf Nolting ambaye ni mmoja wa waandalizi wa Global Media Forum anaeleza jinsi ambavyo mkutano huo unaleta pamoja wataalamu, vyombo vya habari na watumizi wa vyombo hivyo, akisema "Sisi wa DW tumegundua kwamba katika makongamano mengi yanayohusu tabia ya nchi, maendeleo ya kiuchumi ama masuala ya afya, wataalamu huwa wanasisitiza umuhimu wa kuwafikishia wasikilizaji na wasomaji matokeo ya makongamano hayo. Wataalamu wanakubaliana kwamba vyombo vya habari lazima visambaze matokeo ya mikutano hiyo ili kuwapa wananchi wa kawaida nafasi ya kutafuta suluhu ya matizo yaliyopo."

Nolting alisema ana uhakika kwamba waandishi wa habari walioalikwa kwenye Global Media Forum watafanya kazi nzuri ya kuripoti kuhusu yale yatakayojadiliwa. Kwa namna hiyo ujumbe utasambazwa kwa watu duniani kote. Alipoulizwa kuhusu wageni anaofurahia kuwaona alimtaja kwanza Vitali Klitschko, bondia maarufu ambaye sasa amekuwa meya wa mji mkuu wa Ukraine, Kiev. Anausibiri pia ujio wa Scilla Elsworthy, mwanamke aliyeanzisha shirika la utafiti na ambaye ameshapendekezwa mara tatu kupokea tuzo ya amani ya Nobeli.

Kama ilivyo ada, mwaka huu pia washindi wa tuzo ya Bobs watakabidhiwa zawadi zao kwenye kongamano. Tuzo hiyo inatolewa kwa wanablogu bora waliopigiwa kura mtandaoni. Miongoni mwa washindi wa mwaka huu yumo Rafida Bonya Ahmed kutoka Bangladesh. Yeye anaiendeleza kazi ya mume wake, Avijit Roy, mwanablogu aliyeuwawa kikatili Februari mwaka huu akiwa Bangladesh.

Kwa mara ya kwanza kabisa DW itatoa tuzo maalumu kwa ajili ya watetezi wa uhuru wa kutoa maoni. Mwaka huu tuzo hiyo inakwenda kwa mwanablogu Raif Badawai ambaye ametiwa gerezani Saudi Arabia kwa kupigania haki ya kutoa maoni yake.

Mwandishi: Mathias von Hein

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Josephat Charo