1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GOMA:Mapigano yachacha mashariki ya Kongo

20 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7E6

Maelfu ya raia wametoroka makaazi yao kufuatia kutibuka kwa mapigano makali hii leo mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kati ya wanamgambo na waasi wanaongozwa na Generali muasi Laurent Nkunda.

Umoja wa mataifa na jeshi la Kongo wamesema mashambulio mabaya yametokea mapema leo katika eneo la Bunagana mji ulioko kiasi kilomita 50 kaskazini mashariki mwa Goma mji mkuu wa mkoa wa Kivu kaskazini.Kamanda wa jeshi la Kongo Delphin Kahimbi amesema habari walizozipokea zinasema mapigano hayo yanawahusisha wanamgambo wa Mai Mai kutoka Kasereka na wafuasi wa Nkunda.

Msemaji wa kikosi cha Umoja wa mataifa Monuc Sylvie Van Den Wildenberg amesema maelfu ya raia waliojawa na hofu wamekimbilia eneo la Rutshuru kaskazini magharibi mwa Kongo.

Wakati huohuo Uganda imesema imeimarisha vikosi vyake katika mpaka wake na Kongo katika eneo hilo la mapigano ili kujiweka tayari kukabiliana na vikosi vya Nkunda endapo vitaingia eneo hilo.