1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gordon Brown na Jacob Zuma watoa mwito mzozo ukome Zimbabwe

24 Aprili 2008

-

https://p.dw.com/p/Dnew

LONDON

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown na rais wa chama tawala nchini Africa Kusini Jacob Zuma walifanya mazungumzo ya kina hapo jana kuhusu Zimbabwe na kutoa wito wa pamoja wa kumalizika kwa mvutano wa kisiasa kuhusu matokeo ya uchaguzi nchini Zimbabwe na kumtaka rais Robert Mugabe kukubali kutolewa matokeo ya uchaguzi.

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown ametoa mwito wa kukomeshwa kwa ghasia na vitisho dhidi ya upinzani nchini Zimbabwe na kusisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa uamuzi wa raia wa Zimbabwe.Aidha Uingereza imetaka Zimbabwe iwekewe vikwazo vya silaha baada ya taarifa kwamba meli iliyosheheni silaha kutoka China ilikuwa ikijaribu kutafuta bandari ya kutia nanga kwa ajili ya kupeleka silaha hizo nchini Zimbabwe meli hiyo lakini ilikosa bandari na hivyo kulazimika kurejea China.

Chama cha upinzani nchini Zimbabwe na makundi ya haki za binadamu pamoja na nchi za magharibi zimekishutumu chama tawala Zanu Pf kwa kuanzisha kampeini za ghasia za baada ya uchaguzi ambapo MDC imedai ghasia huenda zikasababisha mauaji ya halaiki madai ambayo yamepingwa vikali na serikali ya Mugabe.Waziri wa sheria Patrick Chinamasa amesema hakuna mauaji yoyote ya kisiasa na madai ya chama cha MDC kwamba kuna mauaji ya halaiki ni uongo mtupu.

Marekani pamoja na Ujerumani zimetoa mwito kwa viongozi wa Afrika kujaribu kuutatua mvutano huo wa kisiasa nchini Zimbabwe.Hapo jana kiongozi wa chama cha Upinzani cha MDC Morgan Tsvangirai akiwa katika ziara ya kutafuta usaidizi kutoka kwa viongozi wa Afrika nchini Msumbiji alipinga pendekezo la kuundwa kwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa wazo ambalo lilichapishwa na gazeti la serikali la The Herald.