1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gordon Brown wa Uengereza yu mashakani

Othman, Miraji5 Agosti 2008

Jee David Miliband atachukua nafasi ya Gordon Brown?

https://p.dw.com/p/Eqsv
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uengereza, David MilibandPicha: AP

Mambo yanazidi kuwa mabaya kwa chama tawala cha Labour huko Uengereza. Chama hicho mnamo miezi michache iliopita kimeshindwa mara tatu katika chaguzi ndogo za bunge, ukiwachia pia kupoteza wadhifa wa umeya wa jiji la London, na sasa watu fulani ndani ya chama hicho wanamuandama kiongozi wake, waziri mkuu wa sasa, Gordon Brown. Watu hao ni wale wale waliokuwa waaminifu na wa karibu kwa waziri mkuu aliyepita, Tony Blair. Kuna hati ambayo karibuni ilichapishwa ndani ya gazeti la Mail on Sunday ambapo Tony Blair alinukuliwa akionya kwamba Gordon Brown ameupoteza vibaya umaarufu wa chama hicho miongoni mwa wapigaji kura wa Uengereza. Alionya kwamba siasa za sasa za Gordon Brown zinamrahisishia kiongozi wa chama cha upinzani cha Conservative, David Cameron, kuingia madarakani pindi uchaguzi mkuu utaitishwa wakati wowote kutoka sasa. Gordon Brown amelaumiwa kwa kuwa na kiburi, kukosa fikra na kushindwa kudhihirisha ajenda yake ya kisiasa kwa ajili ya siku za usoni.

Kuna msemo wa Kiengereza, kama ule wa Kiswahili: Usiwache Mbachao kwa Msala Upitao. Msemo huu una umuhimu na inafaa Chama cha Labour uuzingatie. Hivi sasa katika majira haya ya kiangazi, ambako huko Uengereza bado ni kipupwe, kuna tetesi zilizoenea zinazotaka waziri mkuu Gordon Brown asiyekuwa na bahati abadilishwe na mtu mwengine ambaye atakiokoa chama cha Labour.

Watu wengine wanahisi mtu huyo atakua waziri wa sasa wa mambo ya kigeni, David Miliband, kijana, tena aliye hodari na mwenye msimamo ulio wazi, mwenye fasaha ya kuzungumza na ni sawa kama Barack Obama wa Marekani. Yeye anaonekana kuwa ni mtu atayekuwa mpinzani muwafaka wa kijana mwenzake, David Cameron, kiongozi wa sasa wa Chama cha upinzani cha Conservative na mtu ambaye kutokana na uchunguuzi wa maoni ya watu ana nafasi nzuri ya kumshinda Gordon Brown katika uchaguzi mkuu ujao. David Miliband alichapisha makala katika gazeti la Guardian hivi karibuni juu ya namna ya kumzuwia David Cameron asishinde, na jambo hilo lilitafsiriwa na wahakiki wa mambo kuwa ni tangazo lake la kuanza kampeni ya kutaka kuwa kiongozi wa chama cha Labour. Mwenyewe David Miliband amekanusha jambo hilo, na akasisitiza kwamba Gordon Brown bado ni mtu ambaye atakitoa Chama cha Labour kutoka mzozo wa sasa na kukiongoza hadi ushindi.

Lakini kuna wale wanaomtetea Gordon Brown na kuhoji kwamba kwenda chini umaarufu wa Chama cha Labour hakujaanza tangu pale mwanasiasa huyo alipokuwa waziri mkuu, lakini hata katika wakati wa mtangulizi wake, Tony Blair. kama anavosema Othman Nombamba, mtu anayefuatiliza kwa karibu sana siasa za ndani za Uengereza:

Othman Nombamba , mchunguzi wa siasa za ndani za Uengereza.

Na zaidi ni kwamba Gordon Brown hivi sasa anatawala wakati usiokuwa mzuri kwa Uengereza. Sio makosa yake kwamba Uengereza hivi sasa inajionea kupanda juu ughali wa maisha, bei za nishati zinapanda kila siku, masoko ya kutoa mikopo ya kununulia majumba inapata hasara na ni shida sasa kupata mikopo kutoka kwenye mabenki.


Kwa kawaida, hata wakifanya vizuri, wanasiasa ni nadra kushukiriwa. Lakini hakuna waziri mkuu ambaye amekosa bahati kutoka kwa wapigaji kura kama alivyo Gordon Brown hivi sasa. Wapigaji kura wa Kiengereza wanasahau kwamba shida wanazozipata sasa ni kutokana na hali jumla ya mambo ilivyo duniani. Waengereza washukuru kwamba kutokana na uzoefu wake wa kuwahi kuwa waziri wa fedha, nchi hiyo haijaangukia katika hali ambayo sawa na Marekani inavojionea hivi sas. Bado Gordon Brown anakusudia kuengeza uwekezaji katika sekta za afya, elimu, ulinzi wa mazingira na usalama wa ndani, na ukilinganisha na nchi nyingine za Ulaya, ukosefu wa kazi nchini humo sio mbaya sana.

Pale alipoingia madarakani mwaka jana katika majira ya kiangazi, Gordon Brown alitimiza ile hamu yake ambayo aliificha kwa mwongo mzima ya kutaka kuwa waziri mkuu wa Uengereza. Chama chake cha Labour bado kinamuona kama mtu aliyekinusuru chama hicho kwenda chini kutokana na siasa za Tony Blair za kuvishadidia vita vya Iraq vilivokuwa vikiendeshwa na Rais George Bush wa Marekani. Licha ya kwamba Gordon Brown amewavutia wasomi ,lakini magazeti hayajaonesha huruma kwake, yanampenda zaidi kiongozi wa upinzani, David Cameron, kutokana na mtindo wake wa kuzungumza kwa kutumia vijembe na mzaha.

Nilimuuliza Othman Nombamba, mchambuzi wa siasa za ndani za Uengereza, kama ni wazi chama cha Labour kitashindwa katika uchaguzi ujao, aliniambia hivi:

Na hata kama katika uchaguzi ujao, utakaofanyika mwaka mmoja kutoka sasa, Chama cha Labour kitashindwa, ukweli utabaki kwamba Uengereza ilivyo sasa, sio ile iliokutwa na Chama hicho pale kilipoingia madarakani. Heba ya Uengereza duniani, ukitoa ile hatua ya Tony Blair ya kuiingiza moja kwa moja katika vita vya Iraq, inangara zaidi kuliko kabla ya hapo. Tukumbuke:David Miliband alikuwa kipenzi cha Tony Blair, na Tony Blair, mwaka mmoja uliopita, kwa shingo upande, alimpisha Gordon Brown akalie nyumba Nambari Kumi katika Barabara ya Downing, mjini London, makao makuu ya waziri mkuu. Haitokuwa mshangao, japokuwa hadi sasa hakuna ushahidi, ikiwa David Miliband yumo katika njama za kumn'goa Gordon Brown kutoka madarakani, kwani uasi, au kwa jina chafu, uhaini, na mapinduzi ni vitu vya kawaida katika siasa.

Lakini Othman Nombamba, mfuatiliaji wa siasa za Uengereza, hakubali kama kuna njama inapikwa dhidi ya Gordon Brown: