1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guinea ya Ikweta yaandaa uchaguzi wa rais

24 Aprili 2016

Kiongozi aliyeko madarakani kwa muda mrefu barani Afrika, Rais Teodoro Obiang Nguema, anaonekana kushinda uchaguzi utakaoandaliwa leo nchini Guinea ya Ikweta

https://p.dw.com/p/1IbZq
Teodoro Obiang Nguema Präsident von Äquatorial Guinea
Picha: AP

Rais huyo mwenye umri wa miaka 73 ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 37 sasa, huenda akaongoza kwa muhula mwingine wa miaka saba, ikiwa atashinda uchaguzi katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.

Obiang aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 1979 wakati alimwangusha mjomba wake, ambaye baadaye aliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi. Alinusurika jaribio la mapinduzi lililofanywa na mamluki wa kigeni katika mwaka wa 2004.

Viongozi wa upinzani wanaoishi uhamishoni wanaishutumu serikali mjini Malabo kwa kukiuka haki za binaadamu na kutumia vyombo vya usalama vya serikali katika kuwasumbua na kuwatisha wapinzani, madai ambayo serikali inayakanusha. Makundi ya upinzani yanasema uchaguzi huo unaonekana hautakuwa huru, haki na wazi.

Äquatorial-Guinea Militärparade
Rais Obiang Nguema anaongoza kwa mkono wa chumaPicha: DW/R. Graça

Utawala wa Obiang inashutumiwa vikali na makundi ya haki za binadamu kwa kuukandamiza upinzani pamoja na kukithiri kiwango cha rushwa, madai ambayo yamemshusisha mwanawe wa kiume Teodorin, anayechunguzwa nchini Ufaransa kwa kujipatia mapato katika njia ya haramu. Obiang ameongoza mwezi mmoja zaidi ya mpinzani wake wa karibu, Jose Eduardo dos Santos wa Angola, na miezi kadhaa mbele ya Robert Mugabe wa Zimbabwe. Rais wa Cameroon Paul Biya, ambaye amekuwa madarakani tangu 1982, anakamata nafasi ya nne na anaonekana kutaka kugombea tena muhula mwingine mwaka wa 2018. Kisha sasa anafuatwa na Denis Sassou Nguesso, wa Jamhuri ya Congo, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 32, na Yoweri Museveni aliyeongoza kwa miaka 30 – wote walichaguliwa tena mwaka huu.

Rekodi ya uongozi wa muda mrefu bado inashikiliwa na aliyekuwa rais wa Libya marehemu Muammar Gaddafi, ambaye alitawaal kwa miaka 42, akifuatwa na kiongozi aliyefariki wa Gabon POmar Bongo Ondimba aliyetawala kwa miaka 41, na Gnassingbe Eyadema miaka 38. Mfalme wa Ethiopia Haile Selassie aliongoza kwa miaka 44.

Guinea ya Ikweta iliwahukumu kifungo cha miaka 34 jela mamluki Nick Du Toi kutoka Afrika kusini na Simon Mann kutoka Uingereza kwa jaribio la mapinduzi dhidi ya Obiang Nguema Machi 2004.

Mnamo mwaka wa 2009, Mann na Du Toit walipewa msamaha na kuachiliwa huru kufuatia amri ya Obiang Nguema. Kesi hiyo pia ilimwingiza Mark Thatcher, mwana wa kiume wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher, aliyekiri kuwa na hatia katika mahakama ya Afrika Kusini kwa kufadhili njama hiyo ya mapinduzi, na akapewa kifungo kilichocheleweshwa cha miaka minne.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Sekione Kitojo