1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres akusudia kuiboresha UN

2 Januari 2017

Katibu mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito kwa dunia kulipa kipaumbele suala la amani, ikiwa ni kauli yake ya kwanza baada ya kuchukua madaraka kutoka kwa mtangulizi wake Ban Ki-moon.

https://p.dw.com/p/2V9fu
Antonio Guterres
Picha: picture alliance/AP Photo/S. Wenig

Guterres ambaye ambaye amewahi kuwa waziri mkuu wa Ureno na pia amewahi kufanya kazi kama mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, ameapa kufanya mabadiliko muhimu yanayohitajika ili kurejesha hadhi ya taasisi hiyo kwa kufanya marekebisho ya jinsi Umoja wa Mataifa unavyofanya kazi.

Katika siku za nyuma Guterres alinukuliwa akisema kuwa anachukua nafasi wakati ambapo watu duniani kote wakiwa hawana imani na viongozi wao, pamoja na taasisi nyingine za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa, na kuongeza kuwa anakusudia kutilia mkazo uboreshaji wa maeneo matatu ya kimkakati ambayo yanahitaji mabadiliko. Maeneo hayo ni pamoja na kujenga na kudumisha amani, kufikia maendeleo endelevu na kurekebisha utendaji kazi wa ndani wa umoja huo.

"Katika siku ya kwanza, nina swali moja zito katika moyo wangu, jinsi gani naweza kuwasadia mamilioni ya watu walionaswa katika migogoro na kuhangaishwa kwa kiasi kikubwa na vita visivyo na mwisho. Wanawake, watoto na wanaume wanauwawa, misafara ya misaada nayo inalengwa. Ninawaomba mniunge mkono kujitoa kwa ajili ya amani sasa na siku zote. Tuufanye mwaka 2017 uwe mwaka wa amani" alisema Guterres.

Nigeria Umweltministerin Amina Mohammed
Amina Mohammed naibu katibu mkuu wa Umoja wa MataifaPicha: picture alliance/Photoshop

Guterres aanza kazi kukiwa na changamoto nyingi za kusalama

Guterres anaanza awamu ya kwanza ya miaka mitano ya uongozi wake akiwa anakabiliwa na migogoro nchini Syria, Yemen, Sudani Kusini na Libya huku kukiwa na majanga mengine duniani kama vile ugaidi na mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa upande wake katibu mkuu ambaye amemaliza muda wake Ban Ki- moon, wakati akiwaaga wafanyakazi wa umoja huo, aliwashukuru kwa ushirikiano walioonyesha kwa kipindi chote ambacho amekuwa madarakani.

Suala la Marekani kuunga mkono umoja huo likibaki kuwa ni swali la kujiuliza kutokana na kuwa Marekani ni moja kati ya wanachama wa kudumu  wenye kura ya turufu katika baraza la usalama na inachangia asilimia 22 ya bajeti ya kawaida ya umoja wa mataifa, na asilimia 25 ya bajeti ya vikosi vya kulinda amani.

Guterres anatarajiwa kuanza kazi rasmi siku ya Jumanne(03.01.2017) ambapo atazungumza na wafanyakazi wengine wa Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/DW English/AP/DPA

Mhariri:Iddi Ssessanga