1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres asema mamilioni ya watu bado wanaathiriwa na njaa

Zainab Aziz
13 Oktoba 2017

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amesema wafadhili wameitikia kwa haraka onyo alilolitoa mwezi Februari lakini japo janga la njaa limedhibitiwa, ipo haja ya kuongeza misaada ya kibinadamu. 

https://p.dw.com/p/2lo5d
New York Außenminister Gabriel bei der UN-Vollversammlung
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama kwamba hatari ya njaa inaendelea kuathiri mamilioni ya watu licha ya kuwa mafanikio yamepatikana katika kuidhibiti njaa kwa kiasi fulani. Guterres amesema mamilioni ya watu wanaendelea kuathirika kwa baa la njaa na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ndio wanaoteseka kimwili na kiakili.  Katibu huyo mkuu wa Umoja wa mataifa aliliambia baraza kuu la Umoja wa mataifa kwamba asilimia 80 ya ufadhili wa mpango wa misaada ya chakula inawaendea watu walio katika maeneo yanayokumbwa na migogoro.

Guterres alitoa wito mnamo mwezi Februari wa kupatikana kiasi cha dola bilioni 4.4 kwa ajili ya kuzuia njaa na majanga mengine yanayohusiana na njaa. Katibu huyo wa Umoja wa Mataifa amewashukuru wafadhili walitoa karibu asilimia 70 ya fedha ambazo zimesaidia kusambaza chakula, huduma za afya na misaada mingine kwa watu wapatao milioni 13. Takriban asilimia 60 ya watu milioni 815 wanaoteseka kwa njaa wanaishi katika maeneo hayo yenye migogoro.  Bwana amesema anaamini kuwa taasisi yenye nguvu ya Umoja wa Mataifa bado haijalishughulikia ipasavyo mzizi hasa wa tatizo la njaa.

USA UN-Vollversammlung in New York | Guterres
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Reuters/L. Jackson

Katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, ambako mara kwa mara eneo hilo hushambuliwa na magadi wa kundi la Boko Haram, watu wapatao milioni 8.5 wanahitaji misaada ya kiutu. Umoja wa Mataifa umeripoti kuhusu watu 700,000 ambao si rahisi kuwafikia katika majimbo ya Borno na Yobe na ambao huenda wakawa wanahitaji msaada kwa haraka.

Maeneo mengine yenye matatizo kuweza kuwafikia watu wanaohitaji misaada ni mikoa ya Kati na Kusini mwa Somalia, sehemu ambazo bado zinadhibitiwa au ziko chini ya ushawishi wa kundi lakigaidi la al-Shabab pamoja na makundi mengine  ya waasi wenye silaha. Makundi hayo huwalenga wafanyakazi wa mashirikia ya misaada na mara nyingine huwanyang'anya au hata kuharibu vyakula na bidhaa zingine za misaada. Watu zaidi ya milioni 6 wanategemea misaada hiyo ili kukimu maisha yao.

Takriban watu milioni 20 katika nchi za Sudan Kusini, Somalia, Yemen na Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wamo katika hatari ya kuangamia kwa njaa.  Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley aliliambia Baraza la Usalama kwamba mahitaji ya kibinadamu katika nchi hizo nne yakiendelea bila ya kupatiwa ufumbuzi yanaweza kuwafanya watu wanaoathirika kugeukia makundi yenye misimamo mikali.  Balozi Haley amesema sababu kuu ya ongezeko la njaa huko Yemen, Sudan Kusini , kaskazini mashariki mwa Nigeria, na Somalia ni kwa sababu makundi ya wapiganaji yanazuia misaada isiwafikie wanaoihitaji , Haley amesema fedha za ziada zinahitajika, lakini  pia Baraza la Usalama  linapaswa kuchukua hatua zaidi kuhakikisha kwamba wenye makosa wanawajibishwa.

Mwandishi:Zainab Aziz/APE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman