1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Habusi wa kijerumani Blechschmidt aomba asaidiwe

Oummilkheir23 Agosti 2007

Wataliban wasisitiza hawatamuachia huru kabla ya masharti yao kutekelezwa

https://p.dw.com/p/CH9F
Wakorea wanawalilia walio wao waliouliwa na wataliban
Wakorea wanawalilia walio wao waliouliwa na watalibanPicha: AP

Mjerumani mwenye umri wa zaidi ya miaka 60 aliyetekwa nyara na wataliban pamoja na wafanyakazi wenzake 4 wa kiafghani zaidi ya mwezi mmoja uliopita nchini Afghanistan,ameziomba serikali za mijini Berlin na Kabul zimsaidie.Maombi hayo ameyatowa kupitia kanda ya Video iliyoonyeshwa na televisheni ya Afghanistan.

Hii ni mara ya pili kuonyeshwa kanda ya video ya mhandisi huyo wa kijerumani Rudolf BLECHSCHMIDT na wenzake.Ya kwanza ilirushwa Agosti mosi iliyopita na kituo cha matangazo cha Al Jazira,wiki mbili hivi baada ya kutekwa nyara July 18 iliyopita kusini mwa Afghanistan.

Matamshi takriban ni yale yale.”Nimefungwa,na afya yangu si nzuri” anasema BLECHSCHMIDT,mwenye umri wa miaka 62 ambae hali yake inaonyesha kua mbaya zaidi ikilinganishwa na namna alivyokua katika kanda ya kwanza ya Video.

Katika kanda ya Video ya jana,ameonekana kama yuko milimani , amekata tama,mkono kifuani na hata matamshi anapata shida kuyatamka.

“Nataka serikali ya Afghanistan na Ubalozi wa Ujerumani wafanye kila linalowezekana ili niachiliwe huru haraka” amesema kwa kiengereza akiwa na lafdhi ya kijerumani-lakini sauti yake ilifuatiwa na tafsiri kwa lugha ya dari.

Kanda hiyo ya Video ikawaonyesha baadae waafghani wanne,waliosimama wima.

“Tunataka serikali ya rais Hamid Karzai ituokoe” amesema mmojawao kwa lugha ya kipashtu-lugha ya pili ya nchi hiyo inayotumiwa zaidi na wataliban.”Sie ni waafghani-wataliban pia ni waafghani.” Ameongeza kusema mateka huyo.

“Tunataka pia mabaraza yote mawili ya bunge-Wolsi Jirga na Misharanmo Jirga,spika wa bunge Mohammed Yunus Qanooni na mkuu wa baraza la Senet SEBGHATULLAH MUJADADI wasaidie pia ili tuachiwe huru-Wanabidi wawafikirie watoto wao.”

Wataliban wanashurutisha kila wakati kuwaachia mateka wa kijerumani na kurejeshwa nyumbani wanajeshi elfu tatu wa Ujerumani wanaotumikia kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na NATO-ISAF nchini Afghanistan.

Wataliban hadi sasa wamekua pia wakidai waachiliwe huru wenzao 10 waliotiwa ndani nchini Afghanistan.

Wiki iliyopita wataliban walimfungulia njia mhandisi huyo wa kijerumani ya kuzungumza kwa simu na shirika la habari la Ufaransa AFP-kwa kile walichokitaja kua”sababu za afya.”Wakati ule alikua kila kwa mara akisema yuko milimani pamoja na waliomteka nyara.

Mara mbili wiki hii,wataliban wameshikilia hawatamuachia habusi huyo wa kijerumani kabla ya wenzao kumi kufunguliwa.

Mbali na Rudolf BLECHSCHMIDT na wenzake wanne wa kiafghani,wataliban wanawashikilia wamisionari 19 wa Korea ya kusini,kati ya 23 waliotekwa nyara tangu July 19 iliyopita.Wameshawauwa wawili na kuwaachia huru wanawake wawili wagonjwa,Agosti 13 iliyopita.

Jana watalaiban wametishia tena kuwauwa mahabusi hao ikiwa wafungwa wakitaliban hawataachiwa huru.Hata hivyo wameongeza kusema mhandisi wa kijerumani na wénzake wanne ”wataendelea kushikiliwa” ikiwa masharti yao hayatatekelezwa.

Mhandisi mwengine wa kijerumani aliyetekwa nyara pamoja nao,amepigwa hadi kufa.

Viongozi wa Ujerumani na Afghanistan wameshasema”kamwe hawatazungumza na wateka nyara.”