1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hailemariam Desalegn mrithi wa Zenawi Ethiopia

Admin.WagnerD22 Agosti 2012

Serikali ya Ethiopia imemtangaza rasmi Naibu Waziri Mkuu wake Hailemariam Desalegn kukaimu nafasi ya marehemu Meles Zenawi, na kusema atashikilia wafidha huo hadi wakati wa uchaguzi mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/15uQ8
Haile Mariam DesalegnePicha: CC-BY-SA- World Economic Forum

Taarifa rasmi ya kukaimu nafasi ya Zenawi imetolewa leo na msemaji wa serikali Bereket Simon na kwamba kiongozi huyo ataapishwa ndani ya siku mbili hizi.

Bereket ameliambia shirika la habari la Reuetrs kuwa Hailemariam atamalizia muhula wa miaka mitano wa serikali hiyo na kuwa suala hilo halina mjadala. Bunge la nchi hiyo litakutana katika kipindi cha siku mbili zijazo na kumuapisha kiongozi huyo kuwa Waziri Mkuu mpya.

Chama tawala cha Ethiopian People´s Revolutuonary Demokratic Front kitafanya mkutano mkuu kumtangaza kiongozi anayerithi nafasi ya Zenawi lakini akasisitiza kuwa hakuna hata wazo la kumnyima Hailemariam nafasi hiyo. Hata hivyo Bereket hakusema ni lini mkutano huo utakapofanyika.

Marehemu Meles Zenawi wa Ethiopia
Marehemu Meles Zenawi wa EthiopiaPicha: picture-alliance/dpa

Alipoulizwa na waandishi wa habari kama wajumbe wote wa ngazi za juu wa chama wamempitisha Hailemariam kuwa mrithi wa Zenawi, Bereket alijibu kuwa "hawana tatizo na uamuzi huo."

Hailemariam mwenye umri wa miaka 47 amekuwa naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya kigeni wa taifa hilo tangu mwaka 2010. Amewahi kuwa mshauri maalumu wa Zenawi.

Shaka ya kugombea nafasi

Kumekuwa na uvumi kuwa huenda kukazuka ushindani mkali baina ya viongozi wa chama hicho katika kuwania nafasi hiyo. Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, ameliambia shirika la habari la BBC kuwa hana wasiwasi wowote wa kuzuka mtafaruku wa uongozi nchini Ethiopia.

"Sina wasiwasi kwa sababu naamini kuwa kuna viongozi wengi wengine nchini Ethiopia ambao watapata uungaji mkomo wa viongozi wenzao barani Afrika kuunda utawala wa mpito ambao utakuwa wa wazi kwa jamii." alisema Sirleaf

Rais wa Liberia, Ellen Johnson-Sirleaf
Rais wa Liberia, Ellen Johnson-SirleafPicha: Reuters

Sirleaf aliendelea kusema "ingawa hilo ni jambo ambalo waziri mkuu wa zamani hakuweza kulifanya, lakini chaguo lake lilikuwa ni kuangalia zaidi masuala ya uchumi na maendeleo pamoja na kuwapa huduma bora watu wake. Kwa hivyo sasa jukumu la kufanya mabadilko ya kisiasa litaangukia mikononi mwa mrithi wake, viongozi na watu wa Ethiopia na sote tunatumaini watavishinda vikwazo"

Rambirambi zinaendelea kumiminika Ethiopia

Rambirambi zimeendelea kumiminika nchini Ethiopia ambapo Rais wa Marekani Barack Obama ametuma salamu akisema kuwa mchango wa muda mrefu wa Zenawi katika maendeleo ya Ethiopia unastahili kutambuliwa.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amemuita Zenawi kuwa ni kiongozi wa pekee.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: dapd

Nalo shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limetoa wito kwa utawala ujao kufanya mabadiliko ya sheria ya ugaidi ya mwaka 2009 ambayo imesababisha viongozi mbalimbali wa upinzani na waandishi wa habari kufungwa gerezani kwa miaka mingi.

Watetezi wa haki za binaadamu wamekuwa wakimtuhumu Zenawi kwa vitendo vya kukiuka haki za binaadamu.

Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFPE

Mhariri: Josephat Charo