1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haiti: Zoezi la kuwatafuta manusura lakamilika

Kabogo Grace Patricla23 Januari 2010

Baada ya siku 10, tokea Haiti kutingiswa na tetemeko kubwa la ardhi, zoezi la kuwatafuta walionusurika limesimamishwa, hivi leo.

https://p.dw.com/p/LfAa
Zoezi la kuwaokoa watu, Haiti limesimamishwa baada ya siku 10.Picha: AP
Serikali ya Haiti imekamilisha zoezi la kuwatafuta na kuwaokoa watu waliokwama katika vifusi kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea nchini humo wiki iliyopita. Taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uratibu wa Misaada ya Kibinaadamu, imeeleza kuwa hadi sasa watu 132 wameokolewa wakiwa hai kutoka kwenye vifusi.
Spendengala für Haiti Wyclef Jean
Wyclef Jean mwanamuziki maarufu kutoka Haiti aongoza wana muziki wengine katika tafrija ya kukusanya fedha kuwasaidia watu wa Haiti: "Hope for HaitiPicha: AP
Jana Ijumaa watu wawili waliokolewa wakiwa hai katika mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince, siku 10 baada ya tetemeko hilo kutokea. Watu hao, mwanamke mwenye umri wa miaka 84 na kijana mwenye umri wa miaka 22 walikuwa wadhaifu sana, lakini sasa wanaendelea vizuri. Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa na Jeshi la Marekani ambao ni watoaji wakubwa wa misaada nchini Haiti zimetiliana saini mpango wa kuendelea kutolewa misaada ya dharura. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kiasi watu 100,000 wameuawa katika tetemeko hilo la ardhi na 200,000 wamejeruhiwa na wengine milioni moja wamepoteza makaazi yao.