1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Haitoshi kutoa miito"

18 Aprili 2007

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kwa mara ya kwanza katika historia yake, limezungumzia suala la mabadiliko ya hali ya hewa. Azimio lakini halikupitishwa, vile vile wanachama kadhaa wa baraza hilo waliweka wazi kuwa kwa msimamo wao suala hilo halifai kujadiliwa na baraza hilo. Kwa upande mwingine, athari za ongezeko la joto duniani na jinsi mabadiliko haya yanavyoathiri usalama uliwenguni ni kitu kisichoweza kufichwa tena, anasema Ulrike Mast-Kirschning katika uchambuzi wake.

https://p.dw.com/p/CHFw

Mabadiliko ya hali ya hewa yataathiri sana binadamu, hasa watu wanaoishi katika nchi za Kusini – hakuna mtu anayeweza kuyakanusha haya baada ya ripoti zilizotolewa katika wiki za nyuma. Kuna mipangilio mbali mbali ya matukio ya baadaye. Sehemu fulani zitakosa maji na kwenye sehemu nyingine maji yatazidi kupita kiasi. Kima cha maji ya bahari kitapanda na kuharibu makaazi ya watu wengi, hasa visiwani. Kwengineko, dhoruba, joto na ukame utaharibu ardhi ya kilimo. Inasemekana kuwa robo tatu ya Waafrika wote wanakosa maji ya kunywa. Vita dhidi ya ukimwi havina mwisho. Na huo ndio mwanzo tu wa mwenendo huo.

Wataalamu wanasema kuwa sababu moja ya mzozo wa Darfur ni ukame. Kwa hivyo mzozo huo ni mfano tu wa mizozo itakayoweza kutokea siku za usoni. Uhaba wa chakula na maji utazidisha ukubwa wa mizozo iliyoko pamoja na kusababisha vita vingine vipya. Changamoto kubwa ambazo tayari dunia inakabiliana nazo zitaongezeka, kama vile uhamiaji na rasili mali, anasema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingerezea, Bi Margret Beckett.

Uingereza inapaswa kupongezwa kuanzisha mjadala huo katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Lakini tungependa kusikia zaidi kuliko kubadilishana mawazo, miito au mipango ya kupunguza utoaji wa gesi ya Carbondionxide inayosababisha ongezeko la joto. Bila ya serikali kuchukua hatua sasa hivi, janga la hali ya hewa linatokea. Kwa hivyo haitoshi kutoa miito au kufikiria teknolojia mpya, bali inabidi kuwa na sheria na masharti katika kila nchi.

Balozi wa Uchina katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa alisema yeye kwenye wadhifa wake hafai kupiga vita mabadiliko ya hali ya hewa, na huenda wengine wanaozingatia masharti ya sasa hivi tu wanasema hivyo hivyo. Lakini wale anaofikiria mbele wanasema, baraza hilo ndipo pahala panapofaa zaidi kwa suala hili, kwa sababu ni baraza la usalama linalobeba jukumu kuhakikisha amani ya dunia na usalama – hivyo ndivyo ilivyoandikwa katika hati ya Umoja wa Mataifa. Maneno ya balozi wa Uchina yanaonyesha kuwa Uchina kama mtoaji mkubwa wa gesi chafu haitaki kunyooshewa kidole.

Kwa hivyo, changamoto kwa wahusika sasa ni kuvunja mfumo wa sasa wa mamlaka katika baraza la usalama, kwenye halmashauri ya haki za binadamu na katika vyombo vingine vya Umoja wa Mataifa ili kuupa kipaumbele ulinzi wa mazingira na maisha ya binadamu. Inategemea jumuiya ya kimataifa itashirikiana ili kuzuia janga la hali ya hewa lisitokee.