1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki za binaadamu ni za watu wote lakini...

6 Agosti 2013

Kila binaadamu hapa duniani ana haki ya uhuru na usawa - kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binaadamu. Lakini katika mataifa mengi barani Afrika, utakuta haki hizi zinaendelea kukanyagwa na kukiukwa.

https://p.dw.com/p/19JoQ
Mtoto anaonekana kutoka ndani akichunguza kupitia kidirisha kidogo (LAIF).
Picha: LAIF

Kankou Sakiliba kutoka nchini Mali amelazimishwa kuolewa na mwanamume aliyemzidi umri kwa zaidi ya miaka 40. Licha ya unyama huo uliotendwa na familia yake, bado Kankou hajaweka chuki au kuvunja uhusiano na familia eti kwa kumuacha mumewe. Hata hivyo, hajakata tamaa kwamba huenda siku moja hali hiyo ikabadilika. Mbali na kujifunza mengi kuhusu maisha ya Kankou, wasikilizaji wa Noa Bongo pia wanafahamu kuhusu mashirika yanayopigania haki za wanawake hasa uhuru wa kujichagulia mume pasi na kushurutishwa na familia.

Wasikilizaji pia wanafahamu mengi kumhusu Michael Mamabolo, ambaye juhudi zake zimewahamasisha wakaazi wa kijiji cha Mabanda mjini Johannesburg kupigania haki zao za makaazi bora au kumiliki makaazi hayo. Kisha tunakutana na Ngozi Haruna mwenye umri wa miaka 24 kutoka nchini Nigeria. Ni Mkristo aliyeolewa na Muislamu ambaye haikubali imani yake. Matokeo yake analazimika kuhudhuria ibada kanisani kisiri ili asimkere mumewe. Ngozi analigeukia shirika moja lisilo la kiserikali linalowasaidia watu wanaopigania uhuru wa kuabudu.

Mbali na kuwaelimisha wasikilizaji kuhusu haki za binaadamu, mchezo huu wa Noa Bongo Jenga Maisha Yako kuhusu haki za binaadamu, pia unatoa funzo kuhusu umuhimu wa kuwaheshimu watu wengine. Unatuwama juu ya umuhimu wa kuwasaidia wengine katika kupigania haki zao.

Noa Bongo Jenga Maisha Yako ni vipindi vinavyotayarishwa na Deutsche Welle na vinasikika katika lugha sita ikiwa ni pamoja na Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamhara.