1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna ushahidi wa matumizi ya silaha za Sumu Syria: Hagel

Admin.WagnerD25 Aprili 2013

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema kwamba tahadhari kubwa inapaswa kuchukuliwa kabla ya kufanya uamuzi wowote juu ya madai kwamba serikali ya Syria imetumia silaha za sumu dhidi ya waasi.

https://p.dw.com/p/18NHz
Watu wanaoshukiwa kuathiriwa na silaha za sumu Syria wakitibiwa
Watu wanaoshukiwa kuathiriwa na silaha za sumu Syria wakitibiwaPicha: Reuters

Chuck Hagel aliitoa kauli hiyo mjini Cairo, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake nchini Misri. Ilifuatia madai yaliyotolewa Jumanne na mkuu wa utafiti katika kitengo cha ujasusi ndani ya jeshi la Israel Jenerali Itai Brun, ambaye alisema kuwa taarifa zao za kitaalam zinaonyesha kwamba jeshi la Syria, mara kadhaa mnamo miezi ya hivi karibuni limetumia silaha za sumu dhidi ya wapiganaji waasi.

Chuck Hagel alisema maafisa wa jeshi la Israel hawakumjulisha chochote juu ya taarifa hizo alipoizuru nchi hiyo hivi karibuni. ''Kushuku ni kitu kimoja, ushahidi ni kitu kingine tofauti. Tunapaswa kuwa makini kabisa kabla ya kufanya uamuzi wowote'' Alisema waziri Hagel.

Taarifa za kijasusi

Waziri huyo alisema hiyo haimaanishi kwamba hana imani na taarifa za kijasusi za Israel, na kuongeza lakini kuwa Marekani inategemea ripoti za taasisi zake yenyewe, na kwamba hawezi kutamka lolote zaidi hadi pale atakapopata ripoti kutoka taasisi hizo.

Chuck Hagel (kushoto) akizungumza na makamanda wa jeshi la Misri mjini Cairo
Chuck Hagel (kushoto) akizungumza na makamanda wa jeshi la Misri mjini CairoPicha: Reuters

Kabla ya Israel kutoa shutuma kuwa Syria ilitumia silaha za sumu, Ufaransa na Uingereza zilikuwa tayari zimetoa shutuma kama hizo katika Umoja wa Mataifa mwezi uliopita.

Huku hayo yakiarifiwa, nchini Syria kwenyewe mapigano baina ya jeshi la serikali na waasi yanaendelea. Vyombo vya habari vya serikali mjini Damascus vimetangaza asubuhi ya leo kuwa jeshi la serikali limeuteka mji muhimu wa Otaybah, ambao ulikuwa ukitumiwa na waasi kama njia yao ya kujipatia silaha. Wanaharakati wa upinzani pia wamethibitisha kukamatwa kwa mji huo na vikosi vya serikali.

Pigo kwa waasi

Wachambuzi wanasema kukamatwa kwa mji huo ulio karibu ya Damascus, ni pigo kubwa kwa waasi katika juhudi zao za kuukamata mji mkuu huo. Mnamo miezi ya hivi karibuni, waasi wameviteka vituo kadhaa vya jeshi la serikali kusini mwa Damascus, wakitumia msaada wanaopatiwa na washirika wao kutoka nchi za nje. Vituo hivyo walivyoviteka viko katika eneo muhimu kimkakati, ambalo liko kati ya Damascus na mpaka kati ya Syria na Jordan.

Kwa miezi kadhaa waasi wa Syria wamekuwa wakipata mafanikio kutokana na msaada wa kigeni wanaoupata
Kwa miezi kadhaa waasi wa Syria wamekuwa wakipata mafanikio kutokana na msaada wa kigeni wanaoupataPicha: picture-alliance/AP

Mwezi uliopita, serikali ya rais Bashar al-Assad ilianzisha operesheni kubwa ya kuwafurusha waasi kutoka maeneo yaliyo karibu na Damascus, na yalitumia vikosi maalum kuzishambulia ngome zao katika mitaa ya mji huo ambayo wanaidhibiti.

Wakati huo huo, kiongozi muhimu katika kambi ya upinzani Ahmad Moaz al-Khatib, amekitaka kikundi cha Hezbollah cha nchini Lebanon kuondoa wapiganaji wake kutoka Syria, ili kuepusha kile alichokiita ''kuigeuza vita inayoendelea kuwa ya kimadhehebu''. Katika ujumbe alioutoa kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, al-Khatib alimshauri kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah kutoa mchango wenye faida katika mgogoro unaoendela nchini Syria.

Kikundi cha Hezbollah ambacho ni mshirika wa Iran na wa Rais Bashar al-Assad, kimekanusha madai ya upinzani wa Syria, kuwa kimepeleka wapiganaji kusaidia vikosi vya serikali ya nchi hiyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE/DPEA

Mhariri:Josephat Charo