1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ilivyo duniani kuhusu ugonjwa wa Ukimwi

Miraji Othman24 Novemba 2009

Ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya Ukimwi duniani

https://p.dw.com/p/KeJk
Deborah Landey wa kutoka Kanada, makamo wa mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na Ukimwi duniani, UNAIDS, akiwasilisha ripoti ya shirika hilo Novemba 2, 2005Picha: AP

Maambukizi mpya wa ukimwi yamepungua kwa asilimia 17 duniani kote kutoka mwaka 2001 hadi mwaka jana, hivyo yaonesha kuna maendeleo katika kudhibiti kutapakaa virusi vya ugonjwa huo. Hayo yameelezwa na kundi la Umoja wa mataifa linaloshughulikia ugonwa wa Ukmwi na Virusi vya AIDS. Mkurugenbzi wa shirika hilo la UNAIDS, Michel Sidibe, akiwasilisha ripoti ya mwka ya shirika lake huko Shangai, China, amesema habari nzuri ni kwamba kupungua huko kunatokana, angalau kwa sehemu, na jitihada za kuzuwia kutapakaa Ukimwi.

Hata hivyo, Bwana Sidibe alisema matokeo ya uchunguzi uliofanywa yaonesha mipango ya kuuzuia Ukimwi kusambaa mara nyingi inakosea malengo, na kwamba pindi kazi itafanywa kwa njia bora zaidi na kuzituma rasil mali na mipango kule ambako italeta taathira zaidi, basi maendeleo ya haraka zaidi yanaweza yakafanyika na maisha zaidi yanaweza yakanusurika. Dr. Hiroko Nakatani, afisa wa cheo cha juu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, alisema wao wametiwa moyo na matukeo ya uchunguzi huo. Alisema asilimia 42 ya watu walio na Ukmwi katika mataifa yanayoendelea hivi sasa wanapata matibabu, lakini aliongeza kusema kwamba dunia bado inakabiliana na mitihani mingi katika kupambana na kusambaa virusi vya ugonjwa huo.

Waziri wa afya wa China, Chen Zhu, pia alikaribisha maendeleo yanayotia moyo, lakini akaashiria pengo kubwa ambalo liko katika kugharimia kazi za kupambana na janga la Ukimwi.

Tangu mwaka 2001, pale Tangazo la Umoja wa Mataifa lililotoa nia ya kupambana na balaa la Ukimwi kutiwa saini, maambukizi ya kila mwaka katika nchi za Afrika chini ya Jangwa la sahara yamepungua kwa asilimia 15, au tuseme visa laki nne.

Lakini Afrika chini ya Jangwa la Sahara bado inayo idadi ya juu kabisa ya maambukizi miongoni mwa watu wazima, ikilinganishwa na eneo lolote lingine la dunia, kiwango cha asilimia 5.5, na eneo linalopakana na Bahari ya Caribbean, likiwa la pili kwa idadi ya juu kabisa ya maambukizi-asilimia 1.0.

Uchunguzi wa karibuni umeonesha kwamba wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao katika nchi za Kiafrika, chini ya Jangwa la Sahara, ndio wanaofanya sehemu muhimu ambayo hapo kitambo haijasajiliwa ya maambukizi mengi ya kitaifa. Uchunguzi huo pia umeonesha kwamba kunywa pombe nyingi pia kunaambatanishwa na hatari ya kufanya vitendo vya mapenzi miongoni mwa wanaume na wanawake huko Botswana na mataifa mengine ya Kiafrika. Pia kuna ushahidi kwamba Ukimwi unaweza kuchangia sana katika kifo cha mama wakati wa uzazi, kukitajwa kwamba vifo 50,000, vilivotokea wakati wa uzazi, viliambatanishwa na virusi vya Ukmwi huko Kusini mwa Afrika mwaka jana. Nusu ya vifo wakati wa uzazi huko Botswana na Afrika Kusini vinatokana na watu wanaohusika kuwa na virusi vya Ukimwi.

Mkuu wa UNAIDS, Michel Sidibe, alitaka kuweko muelekeo wa pamoja katika afya na ambao utaleta pamoja afya ya akina mama na ya watoto pamoja na mipango ya AIDS na pia pamoja na mipango ya kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu ili kulifikia lengo la pamoja.

Tangu mwaka 2001, maambukizi ya virusi vya AIDS yamepungua kwa asilimia 25 Mashariki ya Asia, na kwa asilimia 10 Kusini na kusini Mashariki ya Asia. Mashariki ya Ulaya, baada ya kuengezeka sana maambukizi miongoni mwa watumiaji madawa ya kulevya, maambukizi yametulia, bila ya kupanda juu, lakini kuna ongezeko katika baadhi ya mataifa, yakiwemo Bangladesh na Pakistan.

Inakadiriwa kwamba watu milioni 33.4 wanaishi na virusi vya Ukimwi duniani kote, wengi wao wakiwa wenyewe hawajijuwi kama wana virusi hivyo. Mwaka jana watu milioni 2.7 waliambukizwa na virusi hiyo, na milioni 3.2 kufa kutokana na matatizo ya kiafya yanayofungamana na Ukimwi. Asilimia 97 ya maambukizi mepya na asilimia 98 ya vifo mwaka jana vilitokea katika nchi zinazoendelea.

Mwandishi: Miraji Othman/dpa

Mhariri: Mohammed Abdulrahman