1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali inatisha nchini Côte d'Ivoire

Oumilkher Hamidou22 Desemba 2010

Laurent Gbagbo anashikilia kuwa yeye ndie rais na kwamba wanajeshi wa kimataifa wataihama nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/zoFg
Wafuasi wa Laurent Gbagbo wakihudhuria mkutano ulioitishwa na kiongozi wa vijana"Charles Ble Goude mjini AbidjanPicha: Picture-Alliance/dpa

Hali inatisha nchini Côte d'Ivoire ambako kambi ya Alassane Outtara,anaetambuliwa kimataifa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais ,imetoa mwito wa "kutoitii" serikali ya mpinzani wake Laurent Gbagbo inayopuuza vikwazo na shinikizo la jumuia ya kimataifa inayomtaka ang'oke madarakani.

Akihutubia kwa njia ya televisheni jana usiku,Laurent Gbago amesema kwa mara nyengine tena yeye ndie aliyeibuka na ushindi wa uchaguzi wa rais, November 28 iliyopita na kuitaka "tume ya kimataifa" ije Côte d'Ivoire kutathmini uhalalifu wa matokeo ya uchaguzi huo.

Laurent Gbagbo anataka Tume hiyo iongozwe na mwakilishi wa Umoja wa Afrika na iwe na wawakilishi kutoka jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS,Umoja wa Afrika,,jumuia ya nchi za kiarabu,Umoja wa Mataifa,Marekani,Umoja wa Ulaya,Urusi na China.Laurent Gbagbo anaendelea kusema:

"Nnawatolea mwito wananchi wote wa Côte d'Ivoire,wasifanye fujo.Wanajeshi wa Umoja wa mataifa na Ufaransa wataihama haraka Côte d'Ivoire.Niko tayari kuzungumza na upande wa upinzani-pamoja pia na Ouattara na hata waasi wanaomuunga mkono."

Elfenbeinküste UN Soldaten
Vikosi vya Umoja wa mataifa vyapiga doria mjini AbidjanPicha: AP

Kambi ya Alassane Dahman Outtara imeukataa hapo hapo mwito huo na kusema Laurent Gbagbo anaendelea kuihadaa dunia.

Njia ya kuingilia hoteli anakokutikana Allasane Ouattara na serikali yake imefungwa.Haijulikani lakini bado kama waliomo ndani ya hoteli hiyo wanaweza kutoka au la.

Wanadiplomasia mjini Abidjan pia wanahisi mwito huo wa Laurent Gbagbo ni mbinu tuu ya kuvuta wakati.

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa mataifa anaeshughulikia juhudi za amani,Alain Leroy anahisi shughuli za vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa zinazidi kuhatarika nchini Côte d'Ivoire.Ameahidi hata hivyo wataendelea na shughuli zao ambazo ni kuwalinda raia na wakuu wa kisiasa.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amezungumzia "kitisho cha kweli" cha kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wakati huo huo rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa anaongoza mkutano hii leo katika kasri la Elysee kuhusu hali namna ilivyo nchini Côte d'Ivoire.

Mkutano wa viongozi wa taifa na serikali wa jumuia ya Ecowas wanatazmiwa kukutana ijumaa hii mjini Abuja Nigeria kuzungumzia pia hali namna ilivyo katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,reuters

Mpitiaji:Abdul-Rahman