1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Afghanistan

Oumilkher Hamidou14 Septemba 2009

Ben Laden ajitoa kimaso maso

https://p.dw.com/p/Jexs
Rais Barack Obama ameapa kuwashinda nguvu magaidiPicha: AP

Na hivi sasa tunaelekea Afghanistan ambako matokeo kamili ya uchaguzi wa rais wa Agosti 20 iliyopita bado hayajatangazwa,lakini mpinzani wa rais Hamid Karzai anataka duru ya pili iitishwe huku kiongozi wa kundi la magaidi la Al-Qaida,Osama Ben Laden akiwataka wamarekani wakomeshe vita nchini humo .

Katika risala yake aliyoitoa kuadhimisha miaka minane ya mashambulio ya kigaidi ya September 11 nchini Marekani,kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaida,Oussama Ben Laden amewatolea mwito wamarekani waishinikie ikulu ya nchi yao ili ikomeshe vita nchini Irak na Afghanistan,na badala yake wao watasitisha mashambulio yao.

Katika risala hiyo iliyotangazwa katika mtandao wa internet wa As Sahab-kwa mujibu wa kituo cha utafiti cha Marekani dhidi ya ugaidi,Ben Laden anatishia kwa kusema "wataendelea na vita vya maangamizi kutoka kila pembe."Osama Ben Laden anadai rais Barack Obama hana uwezo wa kubadilisha mkondo wa vita akihoji ameangukia mateka wa makundi yanayopigania masilahi yao na hasa makaundi ya kiyahudi.

"Mkiamua kulinda usalama wenu na kuachana na vita,tutakua tayari kuzingatia mtazamo huo"-amesema.

Risala hiyo imetangazwa siku mbili baada ya kuadhimishwa miaka minane ya mashambulio ya September 11 ambapo karibu watu elfu tatu waliuwawa.

Wadadisi wanahisi kiongozi huyo wa mtandao wa kigaidi amedhoofika, anaandamwa na anajaribu kujitoa kimaso maso baada ya hasara waliyolishwa katika maeneo ya kikabila nchini Pakistan.

Nchini Afghanistan kwenyewe uchunguzi uliofanywa na serikali unaonyesha raia 30 na wataliban 69 wameuliwa malori mawili yaliyosheheni mafuta yaliporipuliwa na madege ya NATO kwa amri ya jeshi la Ujerumani Bundeswehr.

Mada ya kuwepo wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan imehanikiza pia katika kampeni za uchaguzi mkuu humu nchini.Mgombea wa kiti cha kansela kutoka chama cha SPD,Frank-Walter Steinemeier ametangaza mpango wa vifungu kumi,akishauri wanajeshi wa Ujerumani warejee nyumbani hadi ifikapo mwaka 2013.

Wakati huo huo mpinzani mkubwa wa rais Hamid Karzai katika uchaguzi wa rais nchini Afghanistan,Abdullah Abdullah,anataka duru ya pili ya uchaguzi iitishwe.

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nchi za nje anakosoa udanganyifu uliofanyika wakati wa uchaguzi huo.

Afghanistan Wahlen
Abdullah Abdullah akihutubia wafuasi wakePicha: AP

"Kwa bahati mbaya kamisheni huru ya uchaguzi haikufanya kazi yake vizuri,wakati wote wa uchaguzi ,kabla na baadae pia."

Visa vya udanganyifu vimeripotiwa na wachunguzi tangu wa ndani mpaka wa kimataifa.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali ya uchaguzi huo wa Agosti 20 iliyopita,baada ya kuhesabiwa asili mia 95 ya kura,rais Hamid Karzai anaongoza kwa asili mia 54.3 akifuatiwa nafasi ya pili na Abdullah Abdullah kwa asili mia 28.1.

Matokeo kamili yalikua yatangazwe September 17,yameakhirishwa lakini ili kuruhusu uchunguzi wa madai ya udanganyifu ufanywe.

Mwandishi :Ommilkheir Hamidou /AFP

Mhariri: Abdul-Rahman