1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Afghanistan

18 Septemba 2009

Wito kwa wanajeshi wa kigeni walioko nchini Afghanistan kujitolea zaidi ndipo waweze kufanikiwa ukizingatia changamoto wanazokabiliana nazo.

https://p.dw.com/p/JjWC
Rais Hamid Karzai wakati akipiga kura mjini Kabul, Afghanistan, tarehe 20 Agosti, 2009.Picha: AP

Wakati huohuo Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amefutilia mbali kauli zinazotoa wito wa awamu ya pili ya uchaguzi kufanyika kwasababu ya madai kwamba hila na udanganyifu uliotokea ulikuwa mwingi.Yote hayo yanatokea ikiwa Afghanistan inasubiri kauli ya Tume ya Uchaguzi ya mshindi rasmi wa uchaguzi wa rais baada ya baadhi ya kura kuhesabiwa upya.

Makamanda wa ngazi za juu wa Uingereza na Marekani wamekiri kuwa vikosi vyao vinakabiliwa na changamoto nchini Afghanistan ila ikiwa watajitolea zaidi watafanikiwa.Akitoa hotuba yake mjini London Kamanda wa Marekani Jenerali David Petraeus anayesimamia vikosi vya Afghanistan alisema jana kuwa hali ya Afghanistan inahitaji vikosi hivyo kujitolea zaidi na ni jambo linalowezekana.Kamanda mwenzake wa Uingereza alisema hii leo kuwa kuwaleta wapiganaji wa Taleban katika meza ya mazungumzo huenda kukasaidia kupunguza ghasia nchini Afghanistan.Kwa mujibu wa takwimu visa hivyo vimeongezeka kwa asilimia 60 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

USA General David Petraeus
Jenerali David PetraeusPicha: AP

Kauli hizo zilitolewa punde baada ya shambulio kubwa la bomu la kujitolea mhanga kutokea mjini Kabul.Shambulio hilo lilisababisha vifo vya wanajeshi sita wa Kitaliana na raia 10 wa kawaida wa Afghanistan.Kufuatia tukio hilo Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi alisema kuwa nchi yake sasa inataka kuipunguza idadi ya vikosi vyake nchini humo ila baada ya kushauriana na washirika wa NATO.

Silvio Berlusconi
Waziri mkuu Silvio BerlusconiPicha: AP

Takwimu zilizopo zimebaini kuwa vifo vya wanajeshi wa kigeni wanaohudumu Afghanistan vimefikia kiasi cha 366 mwaka huu pekee.Jambo hilo limeyafanya mataifa ya Ulaya na Marekani kutathmini upya mchango wao. Marekani kwa upande wake iko mstari wa mbele kupambana na ugaidi nchini Afghanistan na kwa sasa inatathmini uwezekano wa kuviongeza vikosi vyake nchini humo.Rais Obama amesisitiza umuhimu wa kuitathmini hali halisi ya Afghanistan.

Jenerali McChrystall amefanya tathmini yake ya mkakati wa kijeshi nasi pia tunalazimika kuitathmini hali ya raia,diplomasia,maendeleo pia kuyatathmini matokeo ya uchaguzi ndipo tujue mkondo wa kufuata.Dhamira yangu ni kufanikiwa.

Hata hivyo makamanda wa kijeshi wa Marekani na Uingereza wana imani kuwa hatua ya kufanya mazungumzo na wapiganaji wa Taleban itachangia pakubwa katika juhudi za kuisaka amani ya kudumu ya Afghanistan.Kulingana na viongozi hao wa kijeshi wengi ya vijana hao wanaohusika katika mashambulizi hawana makosa yoyote ila wana matatizo ambayo bado hayajasuluhishwa ndipo sasa wanalipiza kisasi.

Kwa upande wake Meja Jenerali Nick Carter atakayesimamia vikosi vya kimataifa katika eneo la kusini mwa Afghanistan ifikapo mwezi Novemba,kuna umuhimu wa kuwa raia wa Afghanistan kuiunga mkono serikali yao badala ya wapiganaji wa Taleban.Kiasi cha wanajeshi laki moja wa Marekani na wale wanaosimamiwa na NATO wanashirikiana na serikali ya Afghanistan kupambana na wapiganaji wa Taleban.Utawala wa Taleban ulingolewa madarakani mwaka 2001.

Kwa upande mwengine Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amefutilia mbali kauli zinatoa wito wa awamu ya pili ya uchaguzi kufanyika kwasababu ya madai kuwa hila na udangayifu uliotokea katika uchaguzi wa Agosti ulikuwa mkubwa sana.

Kulingana na matokeo ya muda yaliyotolewa baada ya baadhi ya kura kuhesabiwa upya Rais Hamid Karzai yuko mstari wa mbele kumpiku mpinzani wake mkuu Abdullah Abdullah.Rais Karzai alisisitiza kuwa sharti ujasiri wa raia wa nchi yake uheshimiwe na watendewe haki wakati uchunguzi wa madai hayo unaendelea.

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya walioko Afghanistan wamesema kuwa huenda zaidi ya robo ya kura zote zilizopigwa zilikuwa na hila.Hata hivyo Rais Karzai alifafanua kuwa hana tatizo lolote ikiwa italazimika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na mpinzani wake mkuu Abdullah Abdullah.Alisisitiza kuwa ataridhia hatua hiyo ili kuinusuru nchi yake wala sio kwasababu ya madai ya hila na udanganyifu.

Mwandishi:Thelma mwadzaya-AFPE/RTRE

Mhariri: Mohamed Abdulrahman