1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Côte d'Ivoire

Oumilkher Hamidou3 Januari 2011

Juhudi za upatanishi zimeshika kasi kuepusha balaa la kumtimuwa kwa nguvu madarakani rais anaemaliza wadhifa wake Laurent Gbagbo

https://p.dw.com/p/zsuZ
Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga apatanisha kwa niaba ya Umoja wa Afrika nchini Côte d'IvoirePicha: AP

Jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, inaongoza juhudi za kuikwamua hali ya mambo nchini Côte d'Ivoire ili kuepukana na balaa la kulazimika kutumia nguvu kumng'owa madarakani Laurent Gbagbo.

Wiki tano baada ya uchaguzi wa November 28, ambao matokeo yake yanayobishwa yamezusha mgogoro uliogharimu maisha ya watu karibu 200, viongozi wanne wa taifa na serikali wanatarajiwa kukutana na Laurent Gbagbo na mpinzani wake, Alassane Ouattara, hii leo mjini Abidjan.

Baada ya juhudi kama hizo kushindwa wiki iliyopita, marais wa Benin, Sierra Leone na Cap Verde kutoka jumuia ya ECOWAS wanarejea tena Abdidjan leo wakifuatana na waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga, ambae ni mjumbe wa Umoja wa Afrika. Mwakilishi huyo wa Umoja wa Afrika amezungumzia "ujumbe wa kuhifadhi demokrasi na uamuzi wa wananchi wa Côte d'Ivoire

"Tutazungumza na pande zote zinazohusika nchini Côte d'Ivoire na tutaandaa ripoti pamoja na kuona vipi tunaweza kusonga mbele.Wananchi wa Côte d'Ivoire wametamka wazi kupitia uchaguzi na sauti yao inahitaji kuheshimiwa."

Sawa na umoja wa Afrika, jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, pia inamtaka Laurent Gbagbo ang'oke madarakani. Imefika hadi ya kutishia kutumia nguvu za kijeshi ikiwa rais huyo aliyemaliza wadhifa wake atakataa kuondoka madarakani, na kama juhudi zote za kidiplomasia zitashindwa.

Nigeria Jonathan Goodluck
Raiws Jonaathan Goodluck wa Nigeria,mwenyekiti wa jumuia ya ECOWASPicha: AP

Mwenyekiti wa jumuia ya ECOWAS, rais Goodluck Jonathan wa Nigeria, ameahidi uamuzi wa jumuia yao utajulikana kuanzia kesho.

Juhudi za upatanishi hazina nafasi ya kufanikiwa-Gbagbo ameshasema "hafikirii kulihama kasri la rais licha ya shinikizo kutoka nje."

Hali inatisha. Na pindi juhudi za upatanishi zikishindwa, kuna hatari ya kuzuka matumizi ya nguvu, mapambano kati ya wananchi wenyewe kwa wenyewe au opereshini ya kijeshi ya nchi za Afrika magharibi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afpo,Reuters

Mpitiaji: Miraji Othman