1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Togo bado ya wasiwasi.

Halima Nyanza8 Machi 2010

Jeshi la Ulinzi nchini Togo jana lilifyatua gesi ya kutoa machozi kutawanya mamia ya waandamanaji, wakati ambao upinzani nchini humo ukipinga matokeo ya Uchaguzi mkuu wa Rais uliofanyika nchini humo wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/MMtk
Rai wa Togo Faure Gnassingbe, ambaye ushindi wake alioupata katika uchaguzi mkuu ulifanyika wiki iliyopita, unalalamikiwa.Picha: AP

Hatua hiyo ya jeshi la Togo ilikuja baada ya Chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Union of Forces fo Change -UFC- kutishia kufanya maandamano makubwa dhidi ya Rais Faure Gnassingbe, kiongozi ambaye kuingia kwake madarakani mara ya kwanza mwaka 2005 pia kulisababisha ghasia zilizosababisha vifo vya mamia ya watu.

Maandamano ya jana, ambayo yaliwashiriki wafuasi wa upinzani kati ya 200 na 300, yalihudhuriwa pia na mgombea wa Urais kutoka chama hicho kikuu cha upinzani, UFC, ambaye ameshindwa katika uchaguzi huo, Jean Pierre Fabre, ambaye ameilaumu Tume ya Uchaguzi nchini humo kwa kupotosha matokeo hayo, katika uchaguzi huo ambao unaonekana ni jaribio la kuleta utawala wa kidemokrasia nchini humo. Nchi hiyo kwa miongo minne ilikuwa ikiongozwa na baba wa Rais Faure Gnassingbe, marehemu Gnassingbe Eyadema.

Amesema utawala uliopo sasa, unaoongozwa na Rais Gnassingbe, umekuwa ukiwatendea vitendo vya kikatili raia na kwamba hayatambui matokeo hayo ya uchaguzi.

Naye kiongozi msaidizi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Togo, Patrick Lawson, amesema kutakuwa na maandamano kila siku.

Kwa mujibu wa matokeo hayo ya uchaguzi wa Rais nchini Togo, ambayo yametangazwa siku ya Jumamosi Rais Faure Gnassingbe ametetea tena nafasi yake hiyo baada ya kupata asilimia 60.9 ya kura zote zilizopigwa, na kumshinda mpianzani wake, Jean Pierre Fabre, aliyepata asilimia 33.94 ya kura zote zilizopigwa.

Wakati huohuo, taarifa iliyotolewa na vyama vya upinzani, imewataka watu kujitokeza kesho katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo kupinga matokeo hayo ya uchaguzi wa Rais.

Mmoja wa wanaharakati anayetaka mabadiliko ya kisiasa nchini Togo, Ayih Folla, amesema iwapo serikali inadhani kuwa tayari mambo yamekwisha, inajidanganya, kwani watajipanga na kufanya maandamano kuonesha kuwa ushindi ni wao.

Wakati upinzani ukisema hivyo, wafuasi wa Rais Gnassingbe nao wameonya kuwa wako tayari kupambana na upinzani wowote dhidi yao.

Wakati hali ikiwa tete bado, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ametaka raia wa nchi hiyo kujizuia na hisia zao pamoja na kuwa watulivu, na kwamba hatua zozote zitakazochukuliwa zifanyike kwa njia iliyo sawa na kufuata sheria.

Uchaguzi huo uliofanyika Alhamisi iliyopita ulimalizika bila ya ghasia zozote kubwa, lakini waangalizi kutoka jumuia ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, waliripoti kuwepo hitilafu za karatasi za kupigia kura, huku wanaharakati kadhaa wa upinzani wakiwekwa kizuizini toka Jumamosi.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Miraji Othman