1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Yemen na mazungumzo ya Brexit Magazetini

Oumilkheir Hamidou
5 Desemba 2017

Hali nchini Yemen, mazungumzo ya kujitenga Uingereza na Umoja wa Ulaya-Brexit na kinyang'anyiro cha kuania madaraka katika chama cha CSU mjini Munich ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2om8A
Jemen Ali Abdullah Saleh, Muammar al-Gaddafi und Hosni Mubarak
Picha: Reuters/A. Waguih

Tunaanzia Yemen ambako wito wa kusitishwa mapigano alioutoa rais wa zamani Ali Abdullah Saleh mwishoni mwa wiki umekuwa chanzo cha kuuliwa kwake. Na waliomuuwa sio wengine isipokuwa wale wale washirika wake wa awali, waasi wa kishia-Huthi, linaandika gazeti la "Südwest-Presse": "Wahuthi hawakuwa na cha kupoteza baada rais wa zamani kutangaza kupitia televisheni jumamosi iliyopita, kuvunjika muungano wa vita dhidi ya Saud Arabia na falme za nchi za kiarabu. Baada ya rais anaeishi uhamishoni Saud Arabia, Abed Rabbo Mansur Hadi kuwaamuru wanajeshi wa serikali wakaukomboe mji mkuu Sanaa, inahofiwa mji huo mashuhuri uliotangazwa kuwa turathi za utamaduni wa dunia utafikwa na balaa kama lile lililoifika miji ya Aden,Taiz, Aleppo, Mossul, Homs na Rakka. Na kwa namna hiyo gurudumu la matumizi ya nguvu na maangamizi linaendelea kubingirika na sasa linaelekea kuimeza Yemen ambayo tangu zama za kale imekuwa ikisifiwa kuwa kivutio kikubwa cha ulimwengu wa kiarabu."

 Kizungumkuti cha Brexit

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wameangazia pia yanayoendelea mjini Brussels ambako waziri mkuu wa Uingereza Theresa May alifika ziarani kuzungumzia jinsi  nchi yake inavyofikiria kujibu masharti ya kujitoa katika Umoja wa ulaya. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaandika: "Waingereza wanaounga mkono kujitenga nchi yao na Umoja wa Ulaya, Brexit watayachukuliaje yaliyofikiwa Brussels watakapojua kwamba waziri mkuu Theresa May yuko tayari kuridhia masharti ya Umoja wa Ulaya? Ikiwa kati ya Jamhuri ya Ireland na Ireland ya kaskazini hakutokuwa tena na ukaguzi mkali wa mpakani, hali hiyo itamaanisha moja kwa moja kwamba eneo la kaskazini linaendelea kuwa sehemu ya soko la pamoja na Ulaya na sehemu pia ya umoja wa forodha, na matokeo yake yatakuwa ghadhabu za wananchi.

Zitaanzia Scottland ambako wapiga kura wake mwaka jana walipiga kura dhidi ya Brexit na kudai  yale yale yatakayowezekana kwa Ireland ya kaskazini yawezekane pia kwao. Scottland pia inataka iendelee kuwa sehemu ya soko la pamoja la Umoja wa Ulaya. Kwa jinsi gani yaliyofikiwa na waziri mkuu Theresa May mjini Brussels yanaweza kumgeukia nyumbani, ni suala la kusubiri na kuona."

Mahasimu wa zamani wageuka kuwa waokozi

Mada yetu ya mwisho magazetini inatupeleka kusini mwa Ujerumani katika jimbo la Bavaria ambako kinyang'anyiro cha kuania madaraka kati ya waziri mkuu Horst Seehofer na mpinzani wake mkubwa Markus Söder kimemalizika kwa Söder kutangazwa kuwa mrithi wa waziri mkuu .Gazeti la Hannoversche Allgemeine linaandika: "Seehofer sio kiongozi wa siku za mbele. Ili kuweza kufanikiwa chama cha Christian Social Union kinahitaji kiongozi imara na sio wawili. Kwamba yeye na hasimu yake wa muda mrefu Söder kufumba na kufumbua wanatakiwa  waunde uongozi "wakupigiwa mfano", hilo si jambo linalowezekana. Wahka miongoni mwa wana CSU kuelekea uchaguzi muhimu wa jimbo hilo msimu wa mapukutiko mwakani utazidi kukuwa badala ya kupungua. Kwa jukwaa la mjini Berlin hali hiyo inamaanisha CSU watazidi kuwa washirika wasiotegemeka kuliko walivyokuwa miaka iliyopita.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlanspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman