1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Yemen ni tete, huku makundi ya kikabila yakielekea Sanaa

2 Juni 2011

Maelfu ya watu wenye silaha kutoka makundi ya kikabila yanayounda jamii ya Wayemen wanaelekea kwenye mji mkuu wa Yemen, Sanaa kwa lengo la kumuunga mkono kiongozi wao Sheikh Sadiq al-Ahmar.

https://p.dw.com/p/11SvK
Sadiq bin Abdullah al-Ahmar akizungumza na afisa polisiPicha: picture-alliance/dpa

Taarifa zilizotolewa hii leo na viongozi wa makundi ya kikabila yanayounda jamii ya Wayemen, zimeeleza kuwa makundi hayo yamepambana na vikosi vya usalama katika eneo la kijeshi umbali wa kilometa 15 kaskazini mwa mji mkuu wa Yemen, Sanaa. Kiongozi mmoja wa makundi hayo ya kikabila, amesema kuwa watu hao wenye silaha wanataka kuingia mjini humo kumuunga mkono kiongozi wao Sheikh Sadiq al-Ahmar.

Mapambano makali yaliyosababisha vifo yaliibuka usiku kati ya wafuasi wa Al-Ahmar na vikosi vya usalama vya Yemen katika eneo la Al-Hasaba, mapigano ambayo wakaazi wa eneo hilo wameyaeleza kama ni mabaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha siku tatu zilizopita. Watu 47 waliuawa jana katika mapambano, baada ya makubaliano kati ya vikosi vya usalama na makundi ya kikabila kuvunjika. Makundi hayo ya kikabila yanadhibiti majengo ya umma kwenye mji wa Sanaa.

Unruhen im Jemen
Askari wa makundi ya kikabila akiweka doria katika mitaa ya SanaaPicha: dapd

Makubaliano hayo yalitangazwa Mei 27 mwaka huu, baada ya wiki moja ya mapigano makali yaliyozuka wakati Rais Ali Abdullah Saleh alipoonya kuhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hata hivyo, Rais Saleh amegoma kusaini mpango uliofikiwa na nchi za Ghuba, wa yeye kuachia madaraka kama inavyodaiwa na waandamanaji. Mwezi Machi mwaka huu, Al-Ahmar aliahidi kuwaunga mkono wafuasi wake ambao wamekuwa wakiandamana tangu mwenzi Januari mwaka huu, wakimtaka Rais Saleh ambaye ameitawala nchi hiyo tangu mwaka 1978, aondoke madarakani.

Mtandao wa habari wa wizara ya ulinzi, umeeleza kuwa makundi hayo ya kikabila jana yalilitwaa jengo karibu na ikulu kusini mwa Sanaa. Watu walioshuhudia wamesema kuwa maelfu ya watu wameukimbia mji wa Sanaa, huku maduka mengi yakiwa yamefungwa na misururu mirefu ikionekana katika vituo vya mafuta ya petroli. Serikali ya Rais Saleh imewashutumu wafuasi wa Al-Ahmar kwa kuvunja makubaliano, lakini duru karibu na Al-Ahmar zinaeleza kuwa vikosi vya Rais Saleh ndivyo vya kulaumiwa kutokana na kulifyatulia risasi eneo la kiongozi huyo wa makundi ya kikabila.

Kwa upande mwingine, jana Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton alisema kuwa mzozo wa Yemen hautamalizika hadi hapo Rais Saleh na serikali yake watakapowapa nafasi wapinzani kuanzisha hatua za mpito wa kisiasa na kufanya mageuzi ya kiuchumi.

Hillary Clinton
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Rodham ClintonPicha: AP

Wakati huo huo, taarifa zinaeleza kuwa wanajeshi wa Yemen wamewafyatulia risasi waandamanaji katika mji wa kusini wa Taiz, ambao wanataka kumalizika kwa utawala wa Rais Saleh wa miaka 33 madarakani, kwenye nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Hata hivyo, hakuna taarifa zozote ambazo zimetolewa hadi sasa kuhusu majeruhi au vifo. Mapema juma hili, mjumbe wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa, alisema kuwa ofisi yake inachunguza taarifa kwamba wanajeshi wamewaua kiasi waandamanaji 50 kwenye mji wa Taiz tangu Jumapili iliyopita.

Aidha, taarifa za hivi punde zimesema kuwa safari za ndege zimesimamishwa katika uwanja wa ndege wa Sanaa kutokana na mapigano kati ya makundi ya kikabila na vikosi vinavyomtii Rais Saleh. Mapigano hayo yameukaribia uwanja huo wa ndege, hivyo kusababisha mamia ya abiria kukwama. Wiki iliyopita, uwanja huo wa ndege ulifungwa kwa muda kutokana na mapigano ya mitaani yaliyosababisha vifo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE,RTRE)
Mhariri: Josephat Charo